Rais wa Kenya William Ruto akiwa na hasira kali ameapa kuwachukulia hatua kali wale anaowaita wapanga njama wa kutaka kumuondoa madarakani kwa njia zisizo halali kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027.
Akizungumza Jumatano katika Kituo cha Polisi cha Kilimani jijini Nairobi baada ya kukagua mradi wa makazi ya maafisa wa polisi, Rais Ruto alisisitiza kuwa hatakubali vurugu kutumiwa kama njia ya kubadili uongozi wa taifa.
"Nataka kuwaambia hao wahuni wanaodhani wanaweza kuondoa serikali hii kwa vurugu na njia haramu kabla ya 2027, wajitokeze, wajaribu," alisema kwa ukali.
“Hii ni nchi ya kidemokrasia, uongozi wa taifa utachaguliwa kupitia kura ya wananchi, si kwa risasi au fujo,” aliongeza.
Rais Ruto alilalamikia kile alichokiita ni mashambulizi ya makusudi dhidi ya serikali yake kwa njia ya vurugu, akijiuliza kwa nini marais waliomtangulia hawakukumbana na hali kama hiyo.
“Wananisemea kuhusu Moi, Kibaki, Uhuru… hawa wote walikuwa marais, kwa nini wakati wao hakukuwa na fujo kama hizi? Mbona sasa? Upuuzi huu lazima ukome,” alisema Rais kwa ukali.
Katika hotuba hiyo ya kihisia, Rais aliapa kutumia "njia yoyote inayopatikana" kulinda usalama wa taifa na kuhakikisha wote wanaosababisha vurugu, ama moja kwa moja au kwa kuwafadhili, wanakabiliwa na mkono wa sheria.
“Wale walioonekana wakiiba mali ya wananchi wote watakamatwa, na tuko mbioni kuwakamata wanaowatuma kufanya hivyo,” alisisitiza.
Ruto aliitaja hali ya kushambuliwa kwa vituo vya polisi kama kitendo cha “kutangaza vita” dhidi ya taifa, akisema hawezi tena kuvumilia vitendo vya namna hiyo.
Kauli hiyo ya Rais imekuja baada ya mfululizo wa maandamano yaliyoshuhudiwa nchini kote, ambayo yamesababisha uharibifu wa mali, mauaji ya waandamanaji, pamoja na tuhuma za kuingizwa kwa makundi ya wahuni waliodhaminiwa kisiasa.