Bei Ya Kitunguu Yapanda Kwa Asilimia 650

Baada ya ukame kukumba maeneo mengi ya nchi, wakulima wengi wa kitunguu waliokuwa wameenda hasara kubwa katika msimu wa Oktoba hadi Desemba waliogopa kupanda.

“Lakini wale wachache waliothubutu kupanda katika msimu wa mvua ya Aprili hadi Juni ndio hawa sasa ambao pato limewashtua kwa utamu na wingi,” akasema.

Kwa sasa, madalali wamefurika mji huo wa Kiawara ambao umejipa sifa ya kuwa makao makuu ya biashara hiyo ya vitunguu.

“Huku kumejaa madalali wa hata nchi za Uganda, Rwanda na Sudan Kusini ambao wamekuja kununua vitunguu ili wakauze kwa faida. Kwa mkulima, bei ni Sh150 na hata hatuamini kwamba ni sisi tunahesabiwa pesa kiasi hicho,” akasema Bi Faith Mugure, mkulima.

Malori yaliyo na usajili wa mataifa jirani yanaonekana katika barabara za Kiawara yakisaka vitunguu huku wakulima walio na ufahamu wa kukwamilia mavuno yao wakisababisha uhaba wa muda na kusukuma bei juu.

“Ninyi ambao hamjui kuingia shambani kujichafua sasa fungueni mikoba yenu mtupe fidia ya kuwalimia. Ni wakati wetu sasa na hii bei naona ikitinga Sh250 kwa kilo katika wiki chache zijazo,” akasema Bw Kiago Njiraini.

Hata hivyo, wakulima wengi walitoa malalamiko yao kuhusu gharama kubwa ya uzalishaji huku kwa mfano, kilo moja ya mbegu kwa sasa ikitinga Sh70,000.

Ekari moja ya mimea ya kitunguu chekundu iko na uwezo wa kutoa kilo 16,000 za mavuno kwa sasa hili likiwa ni pato la Sh2.4 milioni ikilinganishwa na Sh320,000 ambazo mkulima angepata Februari.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii