WAZIRI MKUU,Kassim Majaliwa amesema kuwa Sekta ya madini imeendelea kuwa nguzo ya uchumi nchini ambapo katika mwaka 2022 sekta hiyo imekua kwa asilimia 10.9 na kufikia mchango wa asilimia 10.1 kwenye Pato la Taifa mwaka 2024, ikilinganishwa na asilimia 9.0 mwaka 2023.
Amesema hayo Septemba 22 mwaka huu wakati akizungumza katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Bombambili – Geita, alipokuwa mgeni rasmi katika hafla ya ufunguzi wa Maonesho ya Teknolojia ya Madini Geita
Waziri Mkuu Majaliwa amesema, mchango wa madini katika Pato la Taifa umekuwa ukipanda mwaka hadi mwaka, sambamba na kuimarika kwa mifumo ya usimamizi, ukusanyaji mapato na uwekezaji wa ndani na nje ya nchi.
“Mchango wa Sekta ya Madini katika maendeleo ya Taifa si wa kubeza. Kanda ya Ziwa pekee imejidhihirisha kama kitovu cha madini ya dhahabu, Mkoa wa Geita, na mikoa ya jirani na hivi sasa tunashuhudia miradi mikubwa ya madini ikisaidia upatikanaji wa pato, ajira, ujenzi wa miundombinu ya afya, elimu, kilimo, usafiri na uchukuzi na kuendelea kuhakikisha Watanzania wananufaika zaidi,” amesema Majaliwa.
Aidha, Waziri Mkuu amesisitiza umuhimu wa wadau wa sekta hiyo kutumia maonesho ya Geita kama jukwaa la kuonesha jinsi Sekta ya Madini inavyochangia katika mapinduzi ya kiteknolojia hapa nchini, pamoja na mbinu rafiki za uchimbaji na uhifadhi wa mazingira.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba, amesema kuwa uwepo wa maonesho hayo umekuwa kichocheo cha mageuzi makubwa katika Sekta ya Madini, hususan dhahabu.
Samamba amefafanua kuwa kupitia teknolojia mpya zilizotambulishwa na wadau katika maonesho ya miaka ya nyuma, uzalishaji wa dhahabu umeongezeka kwa kasi na kufikia zaidi ya tani 62 kwa mwaka, ukilinganisha na wastani wa tani 45 miaka michache iliyopita.
“Hii ina maana kwamba teknolojia hizo zimeboresha mbinu za uchimbaji na usimamizi, kupunguza upotevu wa madini, na kuongeza tija kwa wachimbaji wadogo na wakubwa. Pia tumeona ongezeko la viwanda vya kusafisha na kuchakata madini, hali inayoongeza thamani kabla ya kuuzwa,”amesema Mhandisi Samamba.