WATAALAM WA KIMATAIFA WATOA MWELEKEO MPYA WA UCHUMI KATIKA KONGAMANO LA TIA MWANZA
TIA Yasistiza Utafiti na Ubunifu Katika Kuchochea Uchumi – Kongamano la Kimataifa la 4 la Usimamizi wa Biashara na Ukuaji wa Uchumi Lafana Mwanza
Mwanza, 25 Novemba 2025 – Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) leo imeongoza Kongamano la 4 la Kimataifa la Usimamizi wa Biashara na Ukuaji wa Uchumi, lililofanyika katika Ukumbi wa Nyerere, Gold Crest Hotel jijini Mwanza, likiwa na ujumbe mahsusi unaoangazia nafasi ya ubunifu, uvumbuzi na biashara katika kuchochea uchumi endelevu.
Akizungumza kumwakilisha mgeni Rasmi, Benjamin Magai ambaye ni Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali , amesisitiza umuhimu wa kuwekeza katika utafiti wa kisayansi, kama njia ya kutoa suluhisho la changamoto za kijamii na kiuchumi. Akibainisha kuwa utafiti ndio injini ya maendeleo, hasa katika maeneo kama ubunifu, teknolojia, tathmini, miundombinu na mikakati ya maendeleo yenye tija.
Dira ya Maendeleo ya 2050 Yawekwa 
Aidha Magai amesisitiza kuwa kongamano kama hilo linaendana na Safari ya Tanzania ya kuelekea Dira ya Maendeleo 2050, yenye nguzo tatu kuu, ikiwemo Uchumi Imara, Jumuishi na Shindani, Uwezo wa Watu na Maendeleo ya Jamii, pamoja na Uhifadhi wa Mazingira na Ustahimilivu
Dhima: Uvumbuzi, Ubunifu na Biashara kwa Uchumi Endelevu
Kongamano la mwaka huu limebeba kaulimbiu “Uvumbuzi, Ubunifu na Biashara kwa Uchumi Endelevu.” Kaulimbiu hiyo imegawanywa katika mada 11, huku machapisho 41 ya tafiti yakitarajiwa kuwasilishwa.
Prof. Pallangyo alisema kuwa kabla ya mawasilisho ya tafiti, kutakuwa na watoa mada wakuu 8 (Keynote Speakers) kutoka ndani na nje ya Tanzania, ambao ni wabobezi katika nyanja zao. Miongoni mwao ni:
Watoa Mada Wakuu ni kama ifuatavyo:-
Ephias Ruhode (Uingereza) – Amefafanua namna mkakati wa biashara unavyopaswa kuongoza kabla ya teknolojia, hasa katika zama za Akili Bandia (AI) kupitia mada “In the Age of AI, Business Strategy Comes Before Technology.”
Gaoua Abdelouahab (Algeria) – Ameeleza namna mabadiliko ya kidigitali na ujasiriamali yanavyoweza kuwa injini ya mapinduzi ya kiuchumi, akichambua “The Algerian Experience.”
Prof. Oksana Kiseleva (Urusi) – Amesisitiza umuhimu wa Ecosystem za Ubunifu katika kuharakisha maendeleo ya kiuchumi duniani.
Dkt. Collin Kamalizeni (Afrika Kusini) – Amejadili nafasi ya uongozi shirikishi katika kuponya majeraha ya uchumi Kusini mwa Jangwa la Sahara kupitia mada “Reimagining Inclusive Leadership as a Catalyst for Economic Recovery in Sub-Saharan Africa.”
Prof. Tandy Lwoga (Tanzania) – Amezindua mjadala juu ya jinsi ubunifu unavyoungana na ujasiriamali katika muktadha wa mifumo ya kidijitali kupitia mada “Innovation Meets Entrepreneurship: Rethinking Digital Collection Development for the Future-Ready User.” Katika hotuba yake ya ufunguzi, Afisa Mtendaji Mkuu wa TIA, Prof. William Amos Pallangyo, amekumbusha kuwa TIA ni mojawapo ya taasisi kongwe na muhimu nchini katika kutoa elimu ya uhasibu, ugavi na fani nyingine za biashara. Ikiwa na kampasi 8 nchini na zaidi ya wanafunzi 32,000, na taasisi hiyo imeendelea kuimarisha mfumo wa mafunzo unaozingatia umahiri (Competence Based Training – CBET), sambamba na kufanya tafiti na kutoa ushauri wa kitaalam.
Akimkaribisha Profesa Goodluck Urassa kutoa salamu za Bodi, viongozi wote wametia mkazo umuhimu wa TIA kuendelea kuwa kichocheo cha sera na maarifa kwa taifa.
Baada ya mawasilisho ya tafiti, TIA imetangaza kuwa itachapisha kitabu maalum kitakachokusanya mapendekezo ya watafiti juu ya namna bora ya kutatua changamoto katika sekta za biashara na uchumi. Kitabu hicho kitasambazwa kwa wadau muhimu, ikiwemo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kama mchango wa TIA katika kusaidia sera na maamuzi ya maendeleo.
Katika kuunga mkono juhudi za Serikali kukuza utalii, washiriki wa kongamano wamepangiwa kutembelea vivutio vya Jiji la Mwanza. Hii ni sehemu ya mkakati wa kutumia kongamano kama nyenzo ya kuhamasisha utalii wa ndani.
Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii