Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka, leo Februari 20, 2026, amezindua programu maalumu inayolenga kuwaimarisha vijana kiuchumi na kutatua changamoto wanazokabiliana nazo.
Uzinduzi huo umefanyika katika hafla ya kufungua mafunzo ya udereva wa pikipiki na bajaji yanayotolewa na Chuo cha Mwanza RVTSC kwa kushirikiana na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Ilemela, Mheshimiwa William Kafiti.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano ya Kazi, Mheshimiwa Deus Sangu, amesema Serikali imetenga zaidi ya shilingi bilioni 3.8 kwa ajili ya kuwaongezea vijana ujuzi nje ya nchi ili waweze kujipatia kipato na kushindana katika soko la ajira la kimataifa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Mheshimiwa Amir Mkalipa, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, amempongeza Mbunge wa Jimbo la Ilemela kwa kuwezesha mafunzo hayo na kuwataka vijana kuyatumia vyema ili kufikia malengo yao ya maendeleo.
Wakizungumza kwa niaba ya wanufaika wa mafunzo hayo, viongozi wa madereva wa bajaji na pikipiki wameipongeza Serikali kwa kuanzisha mpango huo, wakisema utakuwa chachu ya mafanikio na utaongeza tija katika shughuli zao za kila siku.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime