"Nauona mkono wa Rais Samia" - Ado Shaibu

Katibu Mkuu wa chama cha ACT Wazalendo amesema Ado Shaibu amesema kuwa anauona mkono wa Rais Samia Suluhu Hassan kuelekea uhuru wa habari nchini.


Amesema, kila tawala inacho cha kujivunia na kwamba, katika Awamu ya Rais Samia, miongoni mwa historia yake kama kiongozi wa nchini, ni kuitoa tasnia ya habari gizani.

Ado ametoa kauli hiyo leo Machi 8, 2023, ikiwa ni Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kwamba, Rais Samia amekuwa mfano bora kwa viongozi wanawake ndani na nje ya nchi.

"Unapozungumzia uongozi wa Rais Samia kama mwanamke, tunaweza kuona mifano mingi kipindi cha nyuma kidogo tulikuwa gizani, mnajua nyinyi wenyewe hali ilikuwaje? leo unapozungumzia mafanikio ya mchakato wa Mmabadiliko ya sheria ya huduma za habari, ndani yake unaona msukumo mkubwa wa Rais Samia na katika hili, historia yake ndani ya nchi hii itaandikwa," amesema Ado Shaibu

Amesema, Rais Samia amekuwa imara katika kuangalia haki za kila upande, ameitazama sekta ya habari kama kiongozi wa nchi na akaona kuna tatizo kama ilivyokuwa katika demokrasia ya vyama vingi.

"Na kwamba, hata baada ya kuona tatizo, amechukua hatua na hayo yote ameyafanya kama kutafuta suluhu katika kila upande, namuona kama kiongozi mwanamke jasiri na anayeweza kutolewa mfano" ameongeza Ado Shaibu

Hata hivyo, Ado amesisitiza kwamba haoni sababu hata moja kwa tasnia ya habari kuundiwa Baraza la Habari ambalo litasimamiwa na serikali kwani ndani ya tasnia ya habari kuna watu wenye weledi mkubwa na wenye uwezo wa kujisimamia.

"Kuna mifano katika hili, nakumbuka katika zile vurugu za gesi Mtwara ni weledi wa wanahabari pekee waliomaliza vurugu bila kutumia mtutu wala vitisho, kutokana na weledi wao, walikubaliana na kuandika tahariri ambayo ilizima kabisa vurugu Mtwara, angalia kilichofanyika mwaka jana kwenye Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, Afrika nzima ilikuja Tanzania kusherehekea, wanahabari ndio waliopanga hili na matokeo yake Afrika nzima macho yao yalikuwa Tanzania, acha wanahabari wajisimamie," amesema

Mwanasiasa huyo kijana amesema, ikiwa waandishi wa Kenya wanalo baraza lao la habari lisiloingizwa mikono na serikali sawa na lile la Canada na hata Ghana, amehoji kwani Tanzania isichukue mkondo huo?

Pia amesema, Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977, Ibara ya 18 na 19 zinatambua uhuru wa kujieleza, kutoa mawazo lakini hakuna sheria ya Bunge inayowapa nguvu waandishi kutambulika kisheria kama wanasheria, madaktari hivyo kukosa ulinzi kikatiba.

Anasema, waandishi wakitambulika kwa sheria ya Bunge, watasimamia masuala yao ya weledi na utendaji kazi na wanapokosea, kuadhibiana kupitia kamati za maadili kama ilivyo kwa tasnia nyingine nchini.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii