Mwanamuziki maarufu nchini Marekani Sean “Diddy” Combs
Mwanamuziki maarufu nchini Marekani Sean “Diddy” Combs, mwenye umri wa miaka 55, anakabiliwa na mashtaka mazito ya unyanyasaji wa kingono, ulaghai, usafirishaji wa watu kwa ajili ya ukahaba, na kuendesha mtandao wa uhalifu wa kijinsia, kulingana na taarifa zilizotolewa katika mahakama ya Marekani.
Katika ufunguzi wa kesi hiyo, waendesha mashtaka walidai kuwa Diddy alitumia umaarufu wake, hofu na vurugu kudhibiti wanawake – hususan wapenzi wake wa zamani, akiwalazimisha kushiriki vitendo vya ngono visivyo kwa ridhaa, ambavyo alivirekodi na kuvihifadhi.
Ushahidi wa video unaomuonesha Diddy akimpiga na kumburuta nywele mpenzi wake wa zamani, Cassandra Ventura, katika hoteli moja jijini Los Angeles mnamo mwaka 2016, umekuwa kitovu cha kesi hii. Mlinzi wa hoteli hiyo alithibitisha kuwa video hiyo ni ya kweli, na tayari imesambaa mitandaoni.
Mwendesha mashtaka Emily Johnson alisema kuwa Diddy alikuwa akiwadhibiti wanawake kupitia hofu na ushawishi wa kimuziki, na aliendesha kile alichokiita “freak-offs” — tafrija za ngono ambazo zilitumika kama njia ya unyanyasaji na udhibiti wa kisaikolojia.
Shahidi mwingine, Daniel Phillip, meneja wa zamani wa watumbuizaji, alisimulia kuwa alishinikizwa kushiriki ngono na Bi Ventura kwa zaidi ya saa 10, huku Diddy akitazama na kurekodi. Phillip alisema aliogopa kutoa taarifa polisi kutokana na hofu ya kuuawa au kutekwa, akieleza kuwa Diddy ni mtu mwenye “nguvu kubwa na ushawishi usio wa kawaida.”
Alieleza pia kuwa alishuhudia Diddy akimshambulia Bi Ventura zaidi ya mara moja, na mara moja alimvuta nywele kwa nguvu huku akilia kwa sauti.
Kwa upande wao, mawakili wa Diddy wamesema kuwa video hiyo inathibitisha kuwa mshtakiwa ana “tabia yenye kasoro,” lakini siyo uhalifu wa kuendesha biashara ya ngono. Wakili Teny Geragos alisema, “Unyanyasaji wa majumbani sio biashara ya ngono.”
Kesi hii imevuta hisia za watu duniani kote na inatarajiwa kuendelea leo Jumanne, ambapo Bi Ventura mwenyewe atatoa ushahidi wake.