Wananchi waguswa namna ya utatuzi migogoro mahakamani

WANANCHI mkoani Shinyanga, wameonyesha kuguswa na utaratibu wa usuluhishi wa mashauri ya migogoro mahakamani, wakisema ni wa kipekee na utasaidia kuimarisha mshikamano, kuendeleza undugu na kudumisha amani miongoni mwa jamii.

Wakizungumza na Nipashe jana katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, wananchi hao wamesema utaratibu huo ni mkombozi kwa pande zinazogombana, ambao unatoa fursa ya kutatua migogoro kwa njia ya maelewano badala ya kuendeleza uhasama.

Mmoja wa wananchi hao Abdala Musa, amesema ana mgogoro wa mirathi, na kwamba wako tayari kutatuliwa tatizo lao kwa njia ya usuluhishi, ili kutoharibu mahusiano ya kifamilia.

Abeli Masanja kutoka wilayani Maswa mkoani Simiyu, ambaye ana kesi ya mgogoro wa ardhi, amesema utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi utapunguza gharama za mara kwa mara za kufika mahakamani kusikilia mashauri, na hata kupoteza muda ambao ungeweza kutumika katika shughuli za kiuchumi.

Naye, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga Gadiel Mariki, amesema wiki hiyo ya usuluhishi inalenga kuwafikia wananchi kwa kuwapatia elimu ya utatuzi wa migogoro kwa njia ya mazungumzo, ikiwa ni pamoja na mashauri yaliyopo mahakamani na yale ambayo hayajafikishwa mahakamani.

Amesema shughuli hizo zimefanyika kuanzia Aprili 13 hadi 17, ambako wameanza na utoaji wa elimu kuhusu usuluhishi na faida zake, na leo watatoa ya migogoro ya familia na ndoa, kesho migogoro ya ardhi, Alhamisi ya kibiashara na mikataba, na Ijumaa masuala ya usuluhishi yanayohusiana na amani na usalama.

“Elimu hii hutolewa mwisho  saa mbili asubuhi, na baada ya hapo tunasajili migogoro iliyopo mahakamani na mipya, kisha kuziita pande zote mbili na kuzungumza nao ili kutafuta suluhu kwa njia ya makubaliano,” amesema Mariki.

Ametaja faida za usuluhishi wa migogoro, kuwa husaidia kupunguza muda wa kushughulikia mashauri mahakamani, hupunguza gharama, na huwawezesha wahusika kumaliza migogoro kwa njia ya amani.

Hakimu Mkazi Mwandamizi Mahakama ya wilaya ya Shinyanga Catherine Langau, amesema usuluhishi wa migogoro unafaida kubwa kwa pande zote mbili na kwamba wakishakubaliana pande zote mbili, makubaliano yao yanaandikwa na kuwa kama hukumu, na kila mmoja ataondoka na nakala ya makubaliano yao.

“lengo kubwa la usuluhishi ni kumaliza mashauri kwa wakati na kupunguza mrundikano wa kesi mahakamani ,ili kuleta ustawi bora katika jamii, sababu kusikiliza kesi kwa muda mchache watu watapa nafasi ya kufanya shughuli zingine za kiuchumi,” amesema Catherine.

Amesema, kuendesha kesi kwa mfumo wa kawaida wa mahakama unachukua muda mrefu, gharama zinakuwa kubwa, pia unaleta chuki, tofauti na kufanya suluhu ambapo watu wanapatanishwa na kuwa marafiki.

10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii