Mwanamke Afungwa Mwaka Mmoja Jela kwa Kuiba Mtoto

Mahakama ya Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza imemhukumu mwanamke mmoja, Novina Yoel Kuboja (23), kifungo cha mwaka mmoja jela baada ya kupatikana na hatia ya kumuiba mtoto wa miezi mitatu.

Hukumu hiyo imetolewa leo Machi 30, 2026 na Hakimu Mfawidhi, Mhe. Evod Kisoka, baada ya mshtakiwa kukiri kosa hilo mahakamani na kueleza kuwa alifanya hivyo ili kutoisumbua mahakama.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, Kuboja alitenda kosa hilo Machi 11, 2026 katika kijiji cha Nyamatemele, kata ya Nyehunge, wilayani Sengerema. Alishtakiwa chini ya kifungu cha 169(1)(a) cha Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 (marejeo ya mwaka 2023), kinachohusu kosa la kuiba mtoto.

Awali, Wakili wa Serikali, Rivana Kasinisala, aliieleza mahakama kuwa mshtakiwa alimchukua mtoto huyo wa kiume mwenye umri wa miezi mitatu bila idhini ya wazazi wake, kitendo kilichokiuka sheria za nchi.

Katika utetezi wake, mshtakiwa aliiomba mahakama impunguzie adhabu akidai kuwa alichukua mtoto huyo kwa nia ya kumlea kutokana na kushindwa kupata mtoto wake mwenyewe.

Hata hivyo, upande wa mashtaka ulipinga hoja hiyo ukisisitiza kuwa kitendo hicho ni cha kinyume cha sheria na hakiwezi kuvumiliwa, ukiitaka mahakama kutoa adhabu kali ili kuzuia matukio ya aina hiyo.

Akitoa hukumu, Mhe. Kisoka alisema kuwa mahakama haina budi kuzingatia matakwa ya sheria, hivyo akaamuru mshtakiwa kutumikia kifungo cha mwaka mmoja gerezani.

10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii