Mchekeshaji Eric Omondi Sasa Asema Hatawahi Kuoa Maishani Mwake, Ataja Sababu.

Mchekeshaji Eric Omondi sasa anadai kuwa hatawahi kufunga pingu za maisha kwani anaogopa ndoa na matatizo yake.
Mchekeshaji huyo licha ya kuwa na umri wa takriban miaka 40 amefichua kuwa hajawahi kuliwazia suala la ndoa kwani sio kubwa kwake.
“Sitawahi kuoa mimi. Nina shinda na hili suala zima la ndoa,” Mchekeshaji huyo alisema baada ya kuulizwa swali na mchekeshaji mwenzake Oga Obina.
Eric Omondi anadai kuwa mtazamo wange wa ndoa umechangiwa pakubwa na familia yao visa vya talaka vikiwa vingi katika ukoo wake.
“Anko zangu wote wametalikiana. Kwa hivyo najiuliza, iwapo unaenda katika jumba fulani na watu wanakimbia kutoka huko, utaendelea na safari yako na uingie?” Eric aliuliza.
Majuzi, Eric Omondi aliibua hisia mseto baada ya kudai kuwa hana mtoto yeyote licha ya kukaribia umri wa miaka 40.
Akizungumza katika mahojiano nchi Tanzania , mchekeshaji huyo vilevile aliweka wazi kuwa hana mchumba.
Kimzaha, Omondi aliwarushia mistari wanawake wa Tanzania kumteka kimapenzi iwapo watapendezwa naye.
“Nitakuwa miaka 40 hivi karibuni. Sina mtu, sina mtoto. Nilijaribu kutafuta mke pale ‘Wife Material’, imeshindikana. Wanawake warembo wa Arusha, nikiwachekesha, msinisahau,” Eric Omondi alisema.
Mchekeshaji huyo vilevile alielezea kukatizwa tamaa baada ya kuvunjika kwa penzi lake la Chantal Grazioli, raia wa Italia.
Kwa mujibu wa Omondi, juhudi zake zote zilitupwa kwenye jalala na kumwacha akiwa amevunjika moyo.
“Bado niliachwa hata baada ya kumweka mpenzi wangu kwenye billboard nyingi sana. Kutoka siku hiyo, ninaogopa mapenzi sana. Ilikuwa uchungu sana. Nilifanya kila kitu, nikanunua gari. Nikikumbuka hiyo story ya bango, inaniuma sana. Ilinikosti pesa nyingi sana,” alisema.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii