Jamhuri Yafungua Shauri la Mapitio Kesi ya Uhaini ya Lissu

Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kwa niaba ya Jamhuri amefungua shauri la mapitio juu ya uamuzi wa kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu.

Akiwasilisha taarifa hiyo mahakamani leo, Wakili wa Serikali Mkuu, Renatus Mkude, amesema kuwa shauri la mapitio limeungwa mkono na kiapo cha Wakili wa Serikali Cuthbert Mbilinyi na limewasilishwa katika mifumo rasmi ya Mahakama ya Tanzania Februari 24, 2026.

Mahakama ya Rufaa ya Tanzania Dar es Salaam imepokea shauri hilo kama shauri la mapitio na limepewa namba 7203216/2026.

Mkude ameeleza kuwa chimbuko la mapitio hayo ni shauri la jinai namba 19605/2025 lililokuwa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, mbele ya Jaji Dunstan Ndunguru na wenzake wawili.

Msingi wa rufaa ni uamuzi wa Mahakama ya awali kuwa ushahidi wa ziada wa ACP Amini Mahamba haujakidhi vigezo vya kifungu cha 308 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).

Aidha, Jamhuri imeomba shauri lililopo Mahakama Kuu lisimame hadi mahakama ya rufaa itakapokamilisha uamuzi wake, kama inavyotakiwa kisheria, ili kuhakikisha hatua ya rufaa inafuata utaratibu rasmi.

Hata hivyo shauri hili la mapitio linatarajiwa kuamua hatima ya uhalali wa ushahidi wa ziada uliokuwa umepingwa na upande wa utetezi.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii