Kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, imeahirishwa hadi kesho kufuatia mjadala mzito wa kisheria kuhusu notisi ya upande wa Jamhuri ya kuwasilisha ushahidi mpya.
Upande wa Jamhuri uliieleza Mahakama kuwa uliwasilisha notisi hiyo Februari 20, 2026 kwa mujibu wa kifungu cha 308 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.
Wakili wa Serikali alidai kuwa notisi hiyo inaambatanisha maudhui ya ushahidi wa ziada unaokusudiwa kuwasilishwa, ukiwa ni nyongeza ya ushahidi uliotolewa awali na ACP Amini Mahamba.
Kwa mujibu wa hoja ya Jamhuri, ushahidi huo unalenga kukidhi matakwa ya kifungu cha 308(1), huku kifungu cha 308(4) kikieleza kuhusu ushahidi uliopo kwenye jalada la kesi.
Serikali ilieleza kuwa ACP Mahamba alikuwa mchunguzi wa matukio yaliyotokea wakati na baada ya uchaguzi wa Oktoba 29, 2025, na kwamba maelezo hayo ni muhimu katika kuthibitisha hoja za mashtaka.
Hata hivyo, Tundu Lissu alipinga notisi hiyo akisema haikidhi matakwa ya kisheria.
Alidai kuwa kifungu cha 308(1) kinahusu shahidi mpya ambaye ushahidi wake haukusomwa wakati wa hatua ya awali ya usikilizwaji (committal proceedings), na si kuongeza ushahidi wa shahidi ambaye tayari alishatoa ushahidi wake.
Lissu alisisitiza kuwa notisi hiyo haimtaji shahidi mpya kama inavyotakiwa na kwamba inaonekana kulenga kuongeza ushahidi nje ya wigo wa hati ya mashtaka.
Aidha, alieleza kuwa maelezo yanayohusu matukio ya Oktoba 29, 2025 hayapo kwenye hati ya mashtaka, na akaibua hoja kuwa wakati huo alikuwa mahabusu kwa miezi sita na nusu.
Hivyo alionya kuwa Mahakama ikiruhusu notisi hiyo, itakuwa imefungua “sanduku la Pandora” kwa kuruhusu masuala ambayo hayamo kwenye mashtaka kuingizwa katika shauri hilo.
Hata hivyo Mahakama iliahirisha kesi hiyo hadi kesho kwa ajili ya uamuzi au mwendelezo wa usikilizwaji.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime