Wabunge Marekani Wachunguza Kufichwa Majina Kwenye Nyaraka za Epstein

Wabunge wa Marekani wameanza kupitia nyaraka zisizofichwa za mfanyabiashara marehemu Jeffrey Epstein, huku wakionyesha wasiwasi baada ya kubaini kuwa baadhi ya majina yameondolewa katika toleo lililotolewa kwa umma.

Hatua hiyo inafuatia kupitishwa kwa Sheria ya Uwazi wa Nyaraka za Epstein (EFTA), iliyotaka Wizara ya Sheria ya Marekani kutoa nyaraka zote ilizonazo kuhusu Epstein bila kuficha taarifa kwa lengo la kumlinda mtu dhidi ya aibu, kuharibu sifa au kwa sababu za kisiasa.

Hata hivyo, sheria hiyo iliruhusu kufichwa kwa majina ya zaidi ya waathiriwa 1,000 wa Epstein ili kulinda usalama na faragha yao.

Baada ya kuchambua nyaraka hizo, wabunge wamehoji sababu za kuondolewa kwa majina mengine ambayo hayahusiani na waathiriwa, wakitaka kufahamu kama kuna juhudi za kulinda watu mashuhuri waliotajwa kuhusishwa na mtandao wa Epstein.

Baadhi ya wabunge wamesema hatua hiyo inakiuka dhamira ya sheria ya uwazi, wakisisitiza kuwa umma una haki ya kujua ukweli kamili kuhusu waliokuwa wakihusishwa na mtandao wa Epstein.

Aidha kwa sasa Bunge linaitaka Wizara ya Sheria kutoa maelezo ya kina kuhusu vigezo vilivyotumika kuficha majina hayo na lini toleo kamili litapatikana kwa umma.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii