Mwanamuziki wa muziki wa asili (traditional/fusion) kutoka Kenya, Labdi, ambaye ni miongoni mwa wasanii waliopata fursa ya kutumbuiza katika Tamasha la 23 la Sauti za Busara 2026 lililofanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja, Zanzibar, amezungumzia kwa kina wajibu wa wasanii katika kulinda na kuhamasisha haki za watoto na wanawake kupitia sanaa.
Akizungumza katika mjadala maalum wa wasanii na wadau wa sanaa uliopewa jina “Movers and Shakers”, Labdi aliweka wazi kuwa wasanii wengi hutengeneza muziki bila kuzingatia kama kazi zao zinaweza kudumu kwa muda mrefu au kubeba ujumbe chanya wa kijamii, hususan kwa watoto na wanawake.
“Wasanii wengi tunafanya muziki bila kufikiria mustakabali wa mtoto,” alisema Labdi.
Kupitia kauli mbiu ya UNICEF ya mwaka huu, “Let Them Shine”, Labdi alieleza dhamira yake ya kutumia muziki kama chombo cha mabadiliko ya kijamii. Alitangaza pia mipango yake ya kuandaa Extended Playlist maalum kwa ajili ya watoto, pamoja na kuandika kitabu cha watoto, vitakavyolenga kuelimisha, kuhamasisha ubunifu, na kukuza maadili chanya kwa kizazi kijacho.
Labdi alisisitiza kuwa, ingawa kila msanii ana uhuru wa ubunifu na mtindo wake wa uwasilishaji, ni muhimu kwa wasanii kutafakari kwa kina hadhira wanayolenga na athari za muda mrefu za kazi zao katika jamii.
Kauli ya Labdi imepokelewa kama wito kwa wasanii barani Afrika na duniani kote kutumia sanaa kama jukwaa la kutetea haki za watoto, kuhimiza usawa wa kijinsia, na kuchangia katika kujenga jamii yenye misingi imara ya maadili na utu.