Tamasha kubwa la muziki la kimataifa, Sauti za Busara, linalofanyika visiwani Zanzibar, limeendelea kuthibitisha hadhi yake kama moja ya matamasha makubwa na yenye mvuto mkubwa barani Afrika, baada ya toleo la mwaka 2026 kufanikiwa kuvutia wageni na wasanii kutoka mataifa mbalimbali duniani.
Katika toleo la mwaka huu, mmoja wa nyota wakubwa wa muziki barani Afrika, Salif Keita kutoka nchini Mali, alitarajiwa kuwa miongoni mwa wasanii wakuu waliopaswa kutumbuiza. Hata hivyo, hakufanikiwa kufika Zanzibar kutokana na changamoto za kiafya zilizomkumba ghafla, jambo lililomlazimu kujiondoa katika ratiba ya tamasha hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya tukio hilo, Mkurugenzi wa Tamasha la Sauti za Busara, Journey Ramadhani, alikiri kukosekana kwa msanii huyo, lakini akaeleza kuwa Salif Keita aliwakilishwa na bendi yake pamoja na watoto wake, ambao walitoa burudani ya kiwango cha juu na kufanikisha kwa kiasi kikubwa tamasha hilo la 23.
Journey Ramadhani alisema:
“Kwanza kabisa tunaomba radhi kwa usumbufu wowote uliojitokeza kutokana na kukosekana kwa Salif Keita. Hata hivyo, hakuna kilichoharibika, kwani Sauti za Busara imejipanga kikamilifu kuhakikisha kila jambo linaenda kwa mafanikio. Mabadiliko ya uwanja yamewezesha kupatikana kwa eneo kubwa zaidi, linalotoa nafasi ya kujiachia kwa wageni na mashabiki wa muziki. Kwa kuzingatia hali ya hewa, tunapanga tamasha lijalo kufanyika mwezi wa Machi 2027, kabla ya msimu wa mvua kuanza kwa wingi.”
Aliongeza kuwa kukosekana kwa Salif Keita kulikuwa changamoto kubwa kwa waandaaji, kwani haikuwa rahisi kufanya mabadiliko ya ghafla katika ratiba ya tamasha kutokana na ukubwa na hadhi ya msanii huyo.
Tamasha la Sauti za Busara linaendelea kutambulika kimataifa kama jukwaa muhimu la kukuza muziki wa Afrika, utamaduni, na utalii wa Zanzibar, likichangia kwa kiasi kikubwa katika kuitangaza Tanzania kwenye ramani ya matukio makubwa ya kimataifa ya sanaa na burudani.