Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limetangaza kuwa kuanzia leo Februari 06 mwaka huu waongoza sherehe na matukio (MCs) pamoja na Manju Muziki (DJs) wote wasio na vibali halali vya BASATA hawataruhusiwa kujishughulisha na kazi za sanaa nchini.
Kwa mujibu wa BASATA, hatua hiyo inalenga kusimamia maadili, taaluma na ubora wa sekta ya sanaa pamoja na kuwalinda wadau wanaofuata sheria na taratibu zilizowekwa.
Baraza hilo limesema yeyote atakayekiuka agizo hilo atachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kutozwa faini isiyopungua Sh milioni 1 na isiyozidi Sh milioni 3, au kufungiwa kujishughulisha na kazi za sanaa kwa kipindi kisichopungua miezi sita, au kufungiwa maisha kulingana na uzito wa kosa.
BASATA imewataka MC na DJ wote nchini kuhakikisha wanakamilisha taratibu za kupata vibali halali kabla ya kuendelea na shughuli zao, ili kuepuka adhabu na usumbufu.
Aidha Baraza hilo limesisitiza kuwa litaendelea kufanya ukaguzi katika maeneo mbalimbali ili kuhakikisha agizo hilo linatekelezwa ipasavyo kwa maslahi ya sekta ya sanaa na Taifa kwa ujumla.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime