HOTELI zilizo karibu na maeneo ya ibada jijini Mombasa zimepata
pigo baada ya Mahakama ya Mazingira na Ardhi kubatilisha uamuzi uliokuwa
umewalinda dhidi ya kelele na kutoka makanisa jirani.
Awali, Baraza la Mazingira (NET) katika uamuzi wake wa Novemba
19, 2024, lilipigia debe Darajani Hotel Ltd na Bridge Hotel Ltd kwa kutoa amri
ya kudhibiti kelele kutoka kwa makanisa katika eneo hilo.
Baraza hilo liliagiza makanisa yaliyo karibu kudhibiti sauti za
ibada ili zisivuke mipaka ya majengo yao na kuwasumbua wageni.
Uamuzi huo pia ungeweza kusherehekewa na hoteli nyingine
zinazokumbwa na kelele kutoka makanisa.
Hata hivyo, mnamo Machi 19, Mahakama ya Mazingira na Ardhi jijini Mombasa
ilibatilisha uamuzi huo na kuwaacha viongozi wa makanisa hayo waendelee na
kelele zao.
Mahakama ilisema NET halikuwa na mamlaka ya kisheria kusikiliza
kesi hiyo , na hivyo uamuzi wake wote kuwa si halali bila kujali kama ulikuwa
sahihi au la.
Mahakama pia ilibaini kuwa udhibiti wa kelele hauko tena chini
ya Mamlaka ya Kitaifa ya Usimamizi wa Mazingira (NEMA), na hivyo rufaa zote
zinazohusu masuala hayo haziwezi kushughulikiwa na NET.
Mgogoro huo ulianza hoteli hizo mbili zilipowasilisha
malalamishi, zikilalamikia kelele nyingi kutoka makanisa jirani, yakiwemo Life
Transforming Centre, ambazo zilikuwa zinaathiri biashara yao.
Hoteli hizo ziliishutumu NEMA kwa kutoshughulikia malalamishi
yao chini ya Sheria ya Usimamizi na Uratibu wa Mazingira, na kudai kuwa kelele
hizo zilisababisha kupungua kwa wateja na hasara ya kifedha.
NET ilikubaliana na hoteli na kuamuru makanisa kudhibiti sauti
zao ili zisivuke mipaka ya majengo yao.
Pia iliamuru NEMA kufanya ukaguzi na kuwasilisha ripoti ya
utekelezaji ndani ya siku 90.
Hata hivyo, mahakama hiyo haikutoa fidia kwa hoteli, ikisema
ushahidi wa hasara haukuwa wa kutosha.
Makanisa yalipinga uamuzi wa NET, na kukata rufaa katika
Mahakama ya Mazingira na Ardhi.
Yalisema kuwa NET haikuwa na mamlaka, na udhibiti wa kelele sasa
ni jukumu lililogatuliwa chini ya Katiba ya Kenya.
Pia, yalidai kuwa vipimo vya kelele vilivyotumika havikuwa vya
kuaminika na hawakupewa nafasi ya kutosha kusikilizwa kuhusu gharama za kesi.
Mahakama ya Mazingira na Ardhi ilibaini kuwa rufaa kwa NET
lazima itoke kwenye masuala yaliyo ndani ya mamlaka ya NEMA, kama
inavyoruhusiwa na Kifungu cha 129 cha Sheria ya Usimamizi na Uratibu wa
Mazingira.
Mahakama ilisema kuwa kwa kuwa udhibiti wa kelele hauko tena
chini ya NEMA, NET haikuwa na msingi wa kisheria kusikiliza kesi hiyo.
Mahakama pia ilibainisha kuwa hoja ya kutokuchukua hatua kwa
NEMA bado ina utata wa kisheria.
Hatimaye, mahakama ilikubaliana na rufaa ya makanisa na
kubatilisha uamuzi wa NET kwa ukamilifu.
Uamuzi huu umeondoa ulinzi uliokuwa umetolewa kwa hoteli hizo,
na migogoro kama hiyo sasa italazimika kushughulikiwa kwa mifumo mingine ya
kisheria.