MAMIA ya watu, vijana kwa wazee waliojihami kwa koleo, mawakala waliobeba kitita cha hela na madereva wa malori, wamiliki mashine na wafayabiashara wamefurika Homa Bay baada ya madini yanayoshukiwa kuwa dhahabu kugunduliwa.
Mwezi mmoja uliopita, Kijiji cha Maguje, Homa Bay kilikuwa eneo tulivu ambapo mifugo walikula viwanjani na wakulima kupalilia mimea yao katika msimu wa mvua.
Katika maeneo ambayo awali yalichimbwa ‘murram’, hali imegeuka huku wanaume wakichimba kwa mkono na mashine kufungua mitaro yenye kina kirefu kusaka dhahabu.
Wengine wanatumia nguvu huku wakibeba mawe yaliyochimbwa migongoni kabla ya kuyapakia kwenye pikipiki au malori.
Baadhi ya mawe hayo husafirishwa viwandani ambapo mashine hutenganisa dhahabu na miamba.
Kando ya kware, wanawake ambao mwezi mmoja tu uliopita waliuza mboga na samaki wamefunga biashara zao za zamani.
Wanaamka alfajiri kuandaa chapati, maharage na chai kwa wachimba madini.
Yote yalianza na uvumi uliosambaa kwamba dhahabu imegunduliwa kijijini humo.
John Okello, aliyeteuliwa kuwa mwenyekiti wa kituo cha kuchimba madini alisema uvumbuzi huo ulijiri baada ya wakazi kumwona mwanamke akiokota mawe kwenye kware.
Mwanamke huyo aliokota mawe kwa karibu miezi mitano kabla ya baadhi ya wanakijiji kuanza kuuliza alikoyapeleka.
“Aliyaweka kwenye gunia na kuwalipa wahudumu wa bodaboda kuyapeleka eneo lisilojulikana. Baadaye alifichua kuwa anayapeleka katika kituo cha kusafisha dhahabu,” alisema.
Gunia la madini hayo huuzwa kati ya Sh2000 na Sh5000 kutegemea matokeo ya vipimo vinavyofanyiwa sampuli kutoka eneo hilo.
Baada ya kuona jinsi watu wanavyosaka dhahabu kwa ari, kamati ya dhahabu iliyobuniwa kusimamia kituo hicho ilianzisha sheria za kudhibiti oparesheni hizo.
Miongoni mwake ni masharti kwa wachimbaji madini kuwalipa wamiliki ardhi Sh50,000 kabla ya uchimbaji kuanza.
Maafisa wa serikali bado hawajathibitisha kiwango cha mgodi wa dhahabu au kudhibiti shughuli hizo, huku wasiwasi ukitanda kuhusu usalama, mizozo ya ardhi na uwezekano wa wenyeji kukandamizwa na wafanyabiashara wenye ushawishi mkubwa.