Mchungaji wa Kiprotestanti Ezra Jin, mwanzilishi wa moja ya makanisa makubwa zaidi ya kiinjili yasiyotambuliwa rasmi nchini China, ambaye alikuwa anashikiliwa tangu mwezi Oktoba, ameachiliwa huru, shirika lisilo la kiserikali la haki za binadamu limesema siku ya Jumamosi.
Ezra Jin ambaye pia anajulikana kama Jin Mingri, alianzisha "Kanisa la Zion" mnamo 2007, kikundi huru cha kidini ambacho kilikusanya wafuasi elfu kadhaa haraka. Kutokana na ukubwa wake, kanisa hilo lilivutia umakini wa mamlaka na likavunjwa mnamo mwaka 2018. Hata hivyo, baadaye liliweza kupanuka mtandaoni, likifanya ibada kupitia mikutano kwa nji ya video kwenye Zoom na mikusanyiko midogo katika miji arobaini ya China.
Ezra Jin alikamatwa mnamo Oktoba 2025 kwa "matumizi haramu ya mitandao ya habari," pamoja na wachungaji na waumini katika majimbo kadhaa ya China na mji mkuu, Beijing. "ChinaAid inatoa shukrani zake za dhati kwa kuachiliwa huru kwa mchungaji Ezra Jin aliyekuwa akizuliwa jela, ambaye alifika salama Los Angeles mnamo Julai 4, 2026, baada ya kuachiliwa huru nchini China," shirika hilo lenye makao yake nchini Marekani, ambalo linatetea uhuru wa kidini katika nchi hiyo ya Asia, lilieleza katika taarifa iliyoandikwa siku ya Jumamosi.
"Maafisa wa China wanaripotiwa kumwambia kwamba kuachiliwa kwake kulitokana na majadiliano" kati ya Marais Donald Trump na Xi Jinping, na ilikuwa "ishara njema" wakati wa sikukuu ya kitaifa ya Marekani, ChinaAid ilibainisha. Baada ya mkutano wake huko Beijing katikati ya mwezi Mei na rais wa China, Donald Trump alisema ndani ya Air Force One kwamba amejadiliana naye kuhusu uwezekano wa kuachiliwa kwa mchungaji wa kanisa la Kikristo. Kulingana na vyombo vya habari vya Marekani, mchungaji huyu alikuwa Ezra Jin.
Katiba ya China inatambua rasmi "uhuru wa imani," ikimaanisha uhuru wa kuamini katika dini, lakini haitaji "uhuru wa kidini," ambao una athari kubwa. Chama tawala cha Kikomunisti cha China (CCP) kina wasiwasi kuhusu shirika lolote ambalo linaweza kutishia mamlaka yake, na makundi ya kidini ni miongoni mwao. Kulingana na mashirika yasiyo ya kiserikali, makundi haya ya kidini yanazidi kufuatiliwa.
China ilizindua sheria mpya mnamo mwezi Septemba 2025 zinazosimamia shughuli za kidini kwenye mitandao ya kijamii, ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku mahubiri kwenye mtandao wa kijamii wa WeChat kupitia "matangazo ya moja kwa moja".