Zaidi ya wanafunzi milioni 171 duniani kote waliona shule zao zikivurugwa na matukio yanayohusiana na hali ya hewa mwaka wa 2025, kulingana na ripoti ya UNICEF iliyochapishwa leo Alhamisi, Septemba 10, 2026.
Uchambuzi wa data kutoka nchi 106 unaonyesha kwamba matukio yanayohusiana na hali ya hewa, ikiwa ni pamoja na dhoruba, mafuriko, mawimbi ya joto, ukame, na moto usiodhibitiwa, yalikuwa na athari kubwa kwa elimu ya karibu mwanafunzi mmoja kati ya kumi duniani kote. Kati ya kufungwa kwa madarasa, uharibifu wa shule, muda mdogo wa kufundisha, na kupungua kwa mahudhurio shuleni, hatari ya kuacha shule inazidi kuongezeka na hasa huathiri wasichana.
Mnamo mwaka 2025, matukio ya hali mbaya ya hewa kama vile mawimbi ya joto, dhoruba, na moto wa nyika yalivuruga elimu ya zaidi ya wanafunzi milioni 171 duniani kote, kulingana na ripoti ya UNICEF iliyochapishwa leo Alhamisi, Septemba 10, 2026.
Ingawa hakuna nchi iliyosalimika na mivurugiko hii ya masomo, kuna tofauti kubwa kati ya mabara, kama anavyoeleza Jodie Soret, mkuu wa kitengo cha Mipango na Uhamasishaji cha Unicef Ufaransa. "Ripoti hii pia inatuambia kwamba robo tatu ya watoto walioathiriwa na mabadiliko haya katika masomo yao ni watoto wanaoishi katika nchi za Kusini, ambazo ni masikini zaidi. Hilo linatia wasiwasi. Hata hivyo, nchi tajiri nazo hazijasalimika," anaeleza.
Lakini usawa huu kati ya nchi sio ukosefu pekee wa usawa unaoangaziwa na ripoti hiyo. Baadhi ya watoto huathiriwa zaidi kuliko wengine na kufungwa kwa shule. "Tunajua kwamba baadhi ya watoto ambao shule zao zimevurugika wana uwezekano mkubwa wa kuacha shule. Na mara nyingi, ni wasichana," Jodie Soret anaelezea. "Wakati wasichana hawaendi shule, mara nyingi huanza kufanya kazi, hasa kazi za nyumbani: huenda kuchota maji, na kwa haraka sana, msichana huyo anakuwa wa lazima sana katika familia yake ili iweze kuendelea kuishi."
Wasichana wadogo pia wako katika hatari kubwa ya kuacha shule wazazi wao wanapojitahidi kuwalisha. "Katika hali hiyo, kinachoweza kutokea ni kwamba binti anapewa katika ndoa," Jodie Soret anaongeza.
Kwa ujumla, mishtuko ya tabianchi, ambayo inazidi kuwa ya mara kwa mara na kali kutokana na mabadiliko ya tabianchi, ilikuwa na "athari kubwa kwenye masomo" ya zaidi ya watoto milioni 171 katika nchi 106 mwaka jana, UNICEF inasema, ikibainisha kwamba takwimu hizi zinapaswa kutafsiriwa kwa "tahadhari" kutokana na data isiyokamilika. Kuanzia chekechea hadi shule ya upili, elimu ya mwanafunzi mmoja kati ya kumi iliathiriwa na madarasa yaliyofungwa, shule zilizoharibiwa, au likizo ndefu.
Mnamo 2024, karibu watoto milioni 250 katika nchi 85, au mmoja kati ya saba, walikuwa katika hali hii, kulingana na shirika la Umoja wa Mataifa.