Msanii wa Tanzania Manfongo Aapa Kuongoza Kampeni za Kupinga Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto Kupitia Muziki

Katika Tamasha la Sauti za Busara 2026, msanii wa muziki wa singeli kutoka Tanzania, Manfongo, ametangaza rasmi dhamira yake ya kuanza kufanya kazi za muziki na kampeni za kuhamasisha jamii kupinga ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

 

Kupitia mijadala mbalimbali iliyoandaliwa na jukwaa la Movers and Shakers, Manfongo alitoa ahadi hiyo mbele ya waandishi wa habari, wasanii wenzake na wadau wa maendeleo ya jamii na sanaa. Msanii huyo alisisitiza kuwa anatumia sanaa yake kama chombo cha mabadiliko ya kijamii, akilenga kuelimisha na kuhamasisha jamii kuhusu haki, usalama na ustawi wa wanawake na watoto.

 

“Ninaapa kuhakikisha nafanya wimbo kwa ajili ya watoto na wanawake. Tegemeeni muda wowote,” alisema Manfongo wakati wa mdahalo huo.

 

Tamasha la Sauti za Busara limeendelea kuwa jukwaa muhimu kwa wasanii kuonyesha vipaji vyao huku wakichangia katika mijadala ya kijamii yenye athari chanya. Ahadi ya Manfongo imepokelewa kwa matumaini makubwa, hasa katika kipindi ambacho jamii inaendelea kukabiliana na changamoto za ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto

Kwa mujibu wa waandaaji wa mijadala  kupitia  Movers and Shakers, ushiriki wa wasanii katika kampeni za kijamii ni nyenzo muhimu ya kufikia jamii kwa lugha rahisi na yenye kugusa hisia. Manfongo anatarajiwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo, mashirika ya kiraia na vyombo vya habari ili kuhakikisha ujumbe huu unafika kwa jamii pana ndani na nje ya Tanzania.

 

 

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii