UM walaani 'janga la kibinadamu ambalo lingeweza kuepukika' El-Fasher

Ukatili uliofanywa huko El-Fasher, Sudan, mwezi Oktoba mwaka uliyopita ni "janga la kibinadamu ambalo lingeweza kuepukika," Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ametangaza siku ya Jumatatu, akionya kwamba sasa kuna hatari ukatili kama huo utekelezwe tena huko Kordofan.

Akihutubia Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, Volker Türk alitoa taarifa mpya kuhusu hali huko El-Fasher na kulaani matukio ya kutisha yaliyofuata "wimbi la vurugu kali" zilizoendeshwa na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF), wanamgambo weye silaha, baada ya mji huo kuzingirwa kikatili kwa miezi 18.

"Maelfu ya watu waliuawa katika siku chache tu, na makumi ya maelfu walikimbia kwa hofu," alisema, akisisitiza hitaji la "kuwafikisha wale waliohusika mbele ya sheria na kuhakikisha kwamba hili halitatokea tena."

Usiku wa kuamkia mikutano ya faragha ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu Sudan, Naibu Mjumbe Maalum wa Uingereza katika Umoja wa Mataifa, James Kariuki, alisema: "Ukatili huu wa makusudi unalenga kuzidisha hali ambayo  haivumiliki. Njaa haipaswi kamwe kutumika kama silaha ya vita."

Jeshi la serikali la Sudan na Vikosi vyaMsaada wa Haraka (RSF) viko vitani tangu mwezi Aprili 2023. Mgogoro huu umegharimu maisha ya makumi ya maelfu ya watu, mamilioni wakikimbia makazi yao, na umesababisha moja ya migogoro mibaya zaidi ya kibinadamu duniani.

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa alisema kwamba wakati wa ziara yake ya hivi karibuni nchini Sudan, alikusanya ushuhuda wa moja kwa moja kutoka kwa manusura wa vurugu za El-Fasher na kwamba "mara chache aliwaona watu wakiwa na kiwewe na mshtuko mkubwa kutokana na hali hiyo."

"Waliripoti mauaji ya halaiki na mauaji ya raia, ndani ya jiji na wakati wakitoroka makazi yao," Bw. Türk alisema.

"Manusura pia walielezea marundo ya maiti kando ya barabara zinazoelekea El-Fasher, tukio la mwisho wa dunia ambalo mmoja wao alililinganisha na Siku ya mwisho wa dunia," aliongeza.

Alisema kwamba "ukatili wa kijinsia ulitumika kimfumo kama silaha ya vita na RSF" na kuonyesha kwamba timu yake pia ilirekodi visa vya watoto kuajiriwa na kutumia vitani na RSF.

Bw. Turk alisema matokeo ya ofisi yake yanaendana na tathmini ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC, kwamba "uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu" ulifanywa huko El-Fasher.

Ingawa RSF ilihusika na ukatili uliofanywa huko El-Fasher, alisisitiza kwamba jumuiya ya kimataifa ina jukumu la "kufanya vizuri zaidi."

"Ikiwa tutakaa kimya na kuomboleza wakati majeshi na makundi yenye silaha wakifanya uhalifu wa kimataifa uliotambuliwa wazi, tunaweza tu kutarajia hali mbaya zaidi," alionya.

Bw. Turk alisema kwa sasa "ana wasiwasi sana kuhusu hatari ya ukiukwaji huu na unyanyasaji kurudiwa katika eneo la Kordofan," ambapo mapigano yameongezeka tangu kutetwa kwa El-Fasher katika eneo jirani la Darfur.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii