Mtu Mmoja Afariki, 12 Wajeruhiwa Ajali ya Basi Shinyanga

 Mtu mmoja amefariki dunia na wengine 12 kujeruhiwa kufuatia ajali ya barabarani iliyohusisha basi la abiria na roli, iliyotokea katika eneo la Mnada wa Tinde, wilayani Shinyanga.

Ajali hiyo ilitokea wakati basi la Kampuni ya Kisire lenye namba za usajili T 229 EEL, lililokuwa likisafiri kutoka Kahama kwenda Mwanza, lilipogongana uso kwa uso na roli lenye namba za usajili RAE 849 N kutoka nchini Rwanda, lililokuwa limebeba shehena ya mchele.

Akizungumza katika eneo la tukio, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi amesema basi hilo lilikuwa likiendeshwa kwa mwendokasi alisema dereva wa basi alipofika eneo la Mnada wa Tinde aligonga toroli la matikiti kabla ya kugongana na roli hilo.

Kwa mujibu wa Kamanda Magomi basi hilo lilikuwa na jumla ya abiria 42. Kati yao, 12 walijeruhiwa, ambapo majeruhi watano hali zao ni mbaya na wamepelekwa Hospitali ya Rufaa Mwawaza huku wengine saba wakipatiwa matibabu katika Zahanati ya Tinde.

“Chanzo cha ajali hii ni uzembe wa dereva wa basi la Kisire ambaye hakuchukua tahadhari. Baada ya ajali alikimbia eneo la tukio, na Jeshi la Polisi linaendelea kumtafuta ili achukuliwe hatua za kisheria,” amesema Kamanda Magomi.

Kwa upande wake mmoja wa majeruhi, Robert Daudi, amesema alikuwa akisafiri na watoto wake watatu. Amesema waliposikia kishindo kikubwa ndipo walitambua kuwa wamepata ajali hata hivyo watoto wake wako salama.

Jeshi la Polisi limewataka madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali zinazoweza kuzuilika.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii