Obama na Clinton Wakemea Mauaji ya Raia Minneapolis

Waliokuwa Marais wa zamani nchini Marekani Barack Obama na Bill Clinton, wamewataka Wamarekani kusimama na kulinda kile walichokiita maadili na msingi ya taifa, kufuatia mauaji ya muuguzi wa chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) Alex Pretti aliyepigwa risasi na kuuawa na mawakala wa uhamiaji wa Shirikisho.

Alex Pretti mwenye umri wa miaka 37 aliuawa siku ya Jumamosi wakati maafisa wa Shirikisho walipokuwa wakijaribu kumkamata mjini Minneapolis ambapo tukio hilo linakuja chini ya wiki chache baada ya mauaji ya raia mwingine wa Marekani, Renee Good, mama wa watoto watatu mwenye umri huo huo, aliyepigwa risasi na kuuawa akiwa ndani ya gari lake mapema Januari.

Katika taarifa yao ilieleza kuwa siku ya Jumatatu, Barack na Michelle Obama walisema mauaji ya Pretti ni “msiba wa kuhuzunisha” na wakabainisha kuwa ni ishara ya kushambuliwa kwa maadili ya msingi ya Marekani. Walisema tukio hilo linapaswa kuwa wito wa kuwaamsha Wamarekani wote, bila kujali misimamo ya kisiasa.

Wanandoa hao walikosoa vikali mbinu za Idara ya Usalama wa Nchi (DHS), wakieleza kuwa mawakala wa Uhamiaji na Utekelezaji wa Forodha (ICE), baadhi yao wakiwa wamevaa barakoa, wanatumia mbinu za vitisho, unyanyasaji na uchokozi bila kuwajibishwa, hali inayohatarisha maisha ya raia.

Masaa machache baadaye, Rais wa zamani Bill Clinton naye alilaani matukio hayo, akiyataja kuwa ya kutisha na yasiyokubalika. Alisema viongozi wanawapotosha wananchi kwa kuwaambia wasiamini kile wanachokiona kwa macho yao wenyewe.

Clinton aliwahimiza Wamarekani wanaoamini katika demokrasia kusimama, kuzungumza na kudai uwajibikaji, akisisitiza kuwa taifa hilo ni la wananchi.

Wakati huo huo, umati wa waandamanaji ulikusanyika Minneapolis kupinga uwepo na vitendo vya maafisa wa uhamiaji wa Shirikisho, wakitaka haki na mabadiliko katika utekelezaji wa sheria za uhamiaji.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii