Wanne matatani kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya

MAHAKAMA Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi imewatia washtakiwa wanne matatani baada ya kuwakuta na kesi ya kujibua mbapo wakidaiwa kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroine kilo 1.02 kutoka Stendi ya Mabasi ya Magufuli  Mbezi mkoani jijini Dar es Salaam kuelekea Tanga.

Uamuzi huo umetolewa na Jaji Godfrey Isaya baada ya kusikiliza  upande wa mashtaka ulioongozwa na Wakili wa Serikali Erick Kamala wakati wa kufunga ushahidi wao kwa mashahidi 10 na kuieleza mahakama kuwa hawana shahidi mwingine zaidi.

Washtakiwa hao ni Maliki Maliki, Iddi Nassoro, Ally Jafari na Mwinyi Mgazija, ambao wanadaiwa kutenda kosa hilo Machi 24, 2022, katika eneo la Stendi ya Magufuli, Mbezi.

Akisoma uamuzi huo Jaji Isaya alifafanua kuwa baada ya kupitia ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka mahakama imejiridhisha kuwa washtakiwa wana kesi ya kujibu. 

Mara baada ya uamuzi huo mawakili wa utetezi walieleza namna wateja wao watakavyojitetea.

Wakili Habibu Kassim, anayemtetea mshtakiwa wa kwanza, alidai mteja wake atajitetea mwenyewe chini ya kiapo.

Wakili Nehemiah Nkoko, anayewakilisha mshtakiwa wa pili na watatu, naye alidai wateja wake watajitetea kwa kiapo, huku wakitegemea ushahidi wao binafsi.

Wakili Wilson Ogunde, anayemtetea mshtakiwa wa nne, alidai mteja wake atatoa utetezi wake mwenyewe chini ya kiapo.

Mahakama imepanga kuanza kusikiliza utetezi wa washtakiwa hao tarehe 28 Oktoba mwaka huu.

Katika ushahidi uliowasilishwa na upande wa Jamhuri, Inspekta John Marwa alidai kuwa mshtakiwa wa kwanza, Maliki Maliki, ndiye mfanyabiashara mkuu wa dawa za kulevya, akiwagawia wenzake bidhaa hizo ili wauze.

Kwa mujibu wa Inspekta Marwa, Machi 24, 2022, akiwa na askari wenzake walifanya upekuzi katika Kituo cha Mabasi cha Magufuli, Mbezi na kuwakamata Ally Jafari, Maliki Maliki, na Iddi Nassoro Abdallah wakiwa ndani ya basi la kampuni ya Tashriff lililokuwa linakwenda Tanga.

Alidai kuwa wakati wa upekuzi, walikamata pochi nyeusi iliyokuwa na dawa za kulevya aina ya heroine, simu mbili, pamoja na tiketi mbili za safari. 

Ilidaiwa mahakamani kuwa tiketi hizo zilikuwa na majina ya Ally Jafari na Saidi Saidi (jina linalodaiwa kutumiwa na Iddi Nassoro), zikionesha safari kutoka Dar es Salaam kwenda Tanga siku hiyo hiyo.

"Nilipewa jukumu la kuongoza uchunguzi wa shauri hili. Baada ya kukamilisha uchunguzi, tulibaini kuwa washtakiwa wote wanne wanahusishwa moja kwa moja na biashara ya dawa za kulevya," alidai Inspekta Marwa mbele ya mahakama.

Mahakama sasa inasubiri upande wa utetezi kuwasilisha ushahidi wao ili kutoa nafasi ya hukumu itakayobainisha hatima ya washtakiwa hao katika kesi nzito ya usafirishaji dawa za kulevya nchini.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii