Serikali chini ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kutekeleza mikakati ya kuhakikisha vijana wanapata fursa sawa za kujiletea maendeleo binafsi na kuchangia katika ustawi wa Taifa na jamii kwa ujumla.
Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Bi. Mary Maganga wakati wa Ufunguzi wa Kongamano la siku mbili la Vijana Tanzania linalofanyika kuanzia Oktoba 12 hadi 13 Oktoba mwaka huu Jijini Mbeya katika Ukumbi wa City Park Garden.
Aidha mikakati hiyo itajumuisha uanzishaji wa mifumo ya kitaasisi, kisera, mipango kazi, miongozo na sheria zinazolenga kutatua changamoto zinazowakabili vijana katika nyanja tofauti za kijamii na kiuchumi.
Maganga ameeleza kuwa lengo la kongamano hilo ni kuwajengea vijana ujuzi na uwezo wa kushiriki kikamilifu katika mabadiliko ya kijamii na kiuchumi kukuza ushirikiano na ubadilishanaji wa mawazo, pamoja na kutambua na kuunga mkono mipango na miradi ya vijana inayolenga kuinua uchumi wao.
“Vijana ni nguvu ya mabadiliko na maendeleo katika jamii zetu. Ni lazima tutumie vema nguvu hii kubadilisha dunia kuwa mahali bora kwa ajili ya wote,” amesema Katibu Mkuu huyo.
Hivyo amewataka vijana kutumia kongamano hilo kama fursa ya kujifunza, kubadilishana uzoefu na kujadili changamoto zinazowakabili, ili Serikali iweze kuyachukua maoni yao na kuyatumia kuboresha sera, sheria, kanuni na miongozo kwa manufaa ya Vijana wote nchini.
Sambamba na hilo Bi. Mary amewahimiza vijana kote nchini kujitokeza kushiriki katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29 mwaka huu kwa kuchagua viongozi wanaoakisi matumaini, malengo na ndoto za taifa hili.
Awali Katibu Tawala Mkoa wa Mbeya Rodrick Mpogolo aliwasihi vijana kuendelea kuipenda nchi yao na kujivunia Taifa la Tanzania kwa kuwa ni mahala ambapo kila kijana ana mchango mkubwa wa kuleta maendeleo.
Akizungumza kuhusiana na idadi ya washiriki wa kongaamano hilo Mkurugenzi wa Maendeleo ya Vijana Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi,Vijana,Ajira na Wenye Ulemavu Seleman Mvunye alisema limehusisha zaidi ya vijana 1,500 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.