BOOST yaleta mageuzi makubwa elimu ya msingi

Mratibu wa Mradi wa BOOST kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Ally Swalehe amesema Programu ya BOOST imeendelea kuleta matokeo makubwa katika kuboresha elimu ya awali na msingi tangu kuanza kutekelezwa mwaka wa fedha 2021/2022 huku ikitarajiwa kukamilika mwaka 2026/2027. 

Amesema lengo kuu la programu ni kuboresha ujifunzaji wa Elimu ya Awali na Msingi kupitia meneo makuu matatu, kuimarisha mazingira ya ujifunzaji na ufundishaji, umahiri na utendaji wa walimu darasani, na uzingatiaji wa vigezo vya utawala bora.

Ameeleza kuwa thamani ya programu ni shilingi trilioni 1.12, sawa na dola milioni 500 za Kimarekani, ambapo asilimia 96 ya fedha hutolewa kupitia mfumo wa “lipa kulingana na matokeo” na asilimia 4 hupitia utaratibu wa kugharamia miradi moja kwa moja.

Programu hii inatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, ambapo Wizara ya Elimu hutoa miongozo na viwango, huku TAMISEMI ikiratibu na kusimamia utekelezaji katika ngazi ya Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Akitoa ufafanuzi kuhusu maeneo ya utekelezaji, Swalehe alisema mradi wa BOOST una afua saba, zikiwamo kuboresha miundombinu ya shule. Katika eneo hilo, lengo lilikuwa kujenga vyumba 12,000 vya madarasa sambamba na miundombinu ya usafi na maji, lakini hadi sasa zaidi ya vyumba 15,000 vimejengwa na vingine vinaendelea kukamilika katika shule za awali, msingi na sekondari ili kuwezesha utekelezaji wa Elimu ya lazima ya Miaka 10.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii