Mwenge wa Uhuru umeendelea na mbio zake mkoani Mbeya ambapo asubuhi ya leo umeingia katika Jiji la Mbeya Halmashauri ya mwisho kukimbizwa mwenge huo kwa mwaka huu tangu ulipowashwa mapema mwaka huu.
Mwenge huo umeingia jijini Mbeya ukitokea Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe ambako ulikagua na kuweka mawe ya msingi pamoja na kuzindua miradi ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni tisa.
Akipokea Mwenge huo kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Rungwe Jaffar Haniu ambaye ni mkuu wa wilaya ya Mbeya Solomon Itunda amesema kuwa katika Jiji la Mbeya Mwenge wa Uhuru utakimbizwa umbali wa zaidi ya kilomita 40 ukipitia na kukagua miradi yenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 130.
aidha Itunda amebainisha kuwa miradi itakayopitiwa na Mwenge huo ni ile inayohusu sekta za elimu, afya, barabara, pamoja na miradi ya vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu vinavyonufaika na mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri.
Hata hivyo kwa mujibu wa ratiba Mwenge wa Uhuru unatarajiwa kuzimwa kesho katika Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan ikiwa ni kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa kwa mwaka huu.