TaFF YASISITIZA UADILIFU KATIKA MATUMIZI YA FEDHA ZA RUZUKU

Kaimu Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Misitu Tanzania (TaFF), Dkt. Tuli Msuya amewataka wanufaika wa ruzuku zinazotolewa na Mfuko huo kuwa waadilifu, wawazi na wenye uwajibikaji katika matumizi ya fedha hizo, ili kuhakikisha zinatumika kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Dkt. Tuli ametoa wito huo alipokutana na wanufaika wa ruzuku ya TaFF katika Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma wakati wa ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi na kujiridhisha na matumizi ya fedha zilizotolewa na Mfuko huo.

Amesema kuwa fedha za ruzuku zinazotolewa na TaFF ni fedha za umma, hivyo zinapaswa kutumiwa kwa kuzingatia mikataba na masharti yaliyowekwa kati ya wanufaika na Mfuko, ili kuepuka migogoro na matumizi yasiyokusudiwa.

 “Nawapongeza kwa kupata ruzuku hii, kwani ushindani ni mkubwa na sio kila anayewasilisha mradi hufanikiwa.

Hivyo, zingatieni masharti ya matumizi ya fedha hizi, na pale mnapohitaji ufafanuzi zaidi wasiliana nasi ili kuepuka matumizi mabaya ya fedha za umma,” amesema Dkt. Tuli.

Kwa upande wake Mhasibu wa TaFF John Malemo amewahimiza wanufaika kuhakikisha wanaandaa taarifa sahihi za matumizi ya fedha na kutumia risiti za kielektroniki (EFD) wanapofanya manunuzi ya vifaa kama mizinga ya nyuki na vifaa vya uendelezaji wa misitu.

Amesisitiza pia umuhimu wa kuhifadhi nyaraka zote za kifedha kama hati za malipo na risiti halali zinazotambulika kisheria, ili kurahisisha ufuatiliaji na ukaguzi wa matumizi ya fedha.

Wanufaika wa ruzuku hizo wameeleza shukrani zao kwa Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia TaFF wakisema msaada huo umechochea maendeleo ya miradi yao ya misitu na ufugaji nyuki na kuahidi kutumia fedha kwa uwajibikaji na uadilifu, sambamba na kufuata masharti yaliyomo kwenye mikataba yao.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii