Mkuu wa wilaya ya Nzega mkoani Tabora Mhe. Naitapwaki Tukai amehimiza matumizi ya teknolojia kupitia mfumo wa kidigiti wa e-ardhi katika kupata huduma mbalimbali za sekta ya ardhi nchini.
Amesema kuwa matumizi ya teknolojia kupitia mfumo wa e-Ardhi si hiari bali ni hitaji muhimu katika karne ya sasa ambapo ameongeza kuwa mfumo huo unarahisisha utoaji wa huduma unaimarisha uwazi na uaminifu pamoja na kupunguza gharama na muda wa upatikanaji wa huduma.
Akizindua rasmi Kliniki ya Ardhi Oktoba 18 mwaka huu katika Viwanja vya Community Centre Mkuu wa Wilaya ya Nzega Mhe. Tukai aliipongeza Wizara ya Ardhi kwa ubunifu wa kusogeza huduma karibu na wananchi na kueleza kuwa hatua hiyo inasaidia kuongeza uelewa uwazi na usalama wa milki za ardhi.
"Napenda kutoa rai kwa wananchi wa Nzega kuendelea kujitokeza kwa wingi ili kunufaika na huduma hizi muhimu za umilikishaji kupitia Kliniki ya Ardhi elimu ya mfumo wa e-Ardhi na utatuzi wa migogoro ya ardhi,” alisema Mhe. Tukai.
Akiwasilisha taarifa ya utendaji kazi wa Kliniki hiyo Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Makazi Bw. Deogratius Kalimenze amesema Wizara hiyo inalenga kurasimisha vipande vya ardhi 20,000 katika kata tano za Nzega Mashariki, Nzega Magharibi Nzega Ndogo Kitangiri na Uchama ambapo tangu kuanza kwa Kliniki ya Ardhi Oktoba 15 mwaka huu jumla ya wananchi 458 wamepata huduma za elimu ya matumizi ya mfumo wa e-Ardhi na zaidi ya wananchi 109 wamefunguliwa akaunti kupitia mfumo huo.
Aidha viwanja 85 vimehakikiwa na kutambuliwa hati miliki 173 zikisajiliwa ambapo 103 kati yake zimekabaidhiwa kwa wananchi migogoro 17 imesikilizwa na 8 kati ya hiyo imetatuliwa. Pia mapato ya zaidi ya shilingi milioni 23.3 yamekusanywa kupitia makusanyo ya kodi ya pango la ardhi na ada za umilikishaji ardhi.
Kliniki ya Ardhi katika Halmashauri ya Mji Nzega itahitimishwa Oktoba 26 mwaka huu huku wananchi wa Nzega wakiendelea kupata huduma za umilikishaji, elimu ya e-Ardhi, ushauri wa kitaalamu kuhusu masuala ya ardhi pamoja na utatuzi wa migogoro ya ardhi.