Rais wa Kenya William Ruto amemtunuku aliyekuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo hayati Raila Odinga heshima ya juu zaidi kwa raia
Chief of the Order of the Golden Heart (CGH) ikiwa ni siku moja baada ya mazishi yake.
Ruto ametangaza hatua hiyo leo Jumatatu Oktoba 20 mwaka huu wakati akizungumza katika Uwanja wa Ithookwe Kaunti ya Kitui katika maadhimisho ya Siku ya Mashujaa ambayo huadhimishwa kuwakumbuka wapigania uhuru wa nchi hiyo.
“Raila alikuwa kiongozi mwenye maono, aliyepigania haki na amani ya taifa letu. Tunamtunuku heshima hii kama ishara ya shukurani na kumbukumbu ya mchango wake kwa Kenya,” amesema Rais Ruto.
Tuzo hiyo ni ya juu zaidi nchini Kenya na kwa kawaida hutolewa kwa viongozi waandamizi wa serikali marais wa zamani na watu waliotoa mchango wa kipekee kwa taifa.
Raila alizikwa jana katika makazi yake yaliyopo Kang’oka Jaramogi, Bondo, Kaunti ya Siaya.