Tanzania imeshiriki Kongamano la Tano la Biashara na Uchumi kati ya Uturuki na Afrika (5th Türkey - Africa Business and Economic Forum) ambalo limefunguliwa Oktoba 16 mwaka huu jijini Istanbul na Mhe Prof Dkt Ömer Bolat Waziri wa Biashara wa Jamhuri ya Uturuki na kuhudhuriwa na Mawaziri, Viongozi Waandamizi wa Serikali, Mabalozi, Wafanyabiashara wadau wa Sekta binafsi. Ujumbe wa Tanzania kwenye kongamano hilo umeongozwa na Ndg. Asangye N. Bangu, Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Stakabadhi za Ghala (WRRB), akimwakilisha Mhe. Waziri wa Viwanda na Biashara.
Kongamano hilo ambalo litahitimishwa leo Oktoba 17 mwaka huu litajadili na kuweka mikakati ya pamoja yenye lengo la kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kukuza maendeleo ya sekta za biashara na uwekezaji, kilimo, afya, ujenzi, nishati teknolojia na miundombinu kwa maslahi ya nchi za Afrika na Uturuki.
Aidha ujumbe wa Tanzania kwenye kongamano hilo unatarajia kufanya mikutano ya pembezoni ili kuvutia wawekezaji na wafanyabiashara kuja kuwekeza nchini kwenye miradi ya kimkakati, kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi pamoja na kujadili maeneo mapya ya ushirikiano yenye tija katika kuongeza ushindani na kukuza uchumi wetu.