Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Leo XIV ameikosoa dunia kwa kushindwa kuzuia mamilioni ya watu kufa kwa njaa.
Papa amesema kuruhusu binaadamu wengine wafe kwa njaa ni kushindwa kwa pamoja kuchukua hatua stahiki, ni kupotoka kwa maadili na yote hayo ni dhambi ya kihistoria.
Katika hotuba yake kwenye makao makuu ya Shirika la Mpango wa Chakula Duniani WFP mjini Roma, Papa Leo XIV ametoa wito kwa watu kufikiria upya mtindo wao wa maisha pamoja na vipaumbele vyao.
Kauli ya kiongozi huyo wa kidini imetolewa wakati WFP ikitahadharisha takriban watu milioni 319 wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula na kwamba kuna hatari watu milioni 14 wakafariki kwa njaa kufikia mwaka 2030, kutokana na hatua ya mataifa kadhaa kupunguza ufadhili kwa ajili ya misaada ya kibinaadamu.