WANAWAKE VIJIJINI WAHIMIZWA KUENDELEZA MIFUMO ENDELEVU YA CHAKULA

Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Chakula Duniani Oktoba 15 mwaka huu yameendelea kwa shamrashamra mbalimbali mkoani Tanga huku Wananchi na Wadau wa Maendeleo na Taasisi za Kilimo wakijumuika kusherehekea Siku ya Mwanamke Kijijini.

Tukio hilo limebeba ujumbe wa kuhamasisha matumizi ya vyakula na mbegu za asili, pamoja na kutambua mchango mkubwa wa wanawake vijijini katika uzalishaji na uhifadhi wa chakula nchini.

Viongozi na Wadau wa Maendeleo wameeleza kuwa wanawake vijijini wana mchango muhimu katika kuhakikisha usalama wa chakula hivyo ni lazima kuendelea kuwawezesha kupitia elimu, teknolojia na upatikanaji wa masoko ya uhakika.

Maadhimisho haya yameambatana pia na sherehe za kutimiza miaka 80 ya Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO), shirika ambalo limeendelea kuwa mshirika wa karibu wa Serikali katika kuimarisha Sekta ya Kilimo, lishe na mifumo endelevu ya chakula nchini.

Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imeendelea kusisitiza dhamira yake ya kuendeleza ushirikiano na mashirika ya kimataifa kama FAO, ili kuhakikisha wanawake vijijini wanapata fursa sawa katika Sekta ya Kilimo na kuchochea maendeleo endelevu ya mifumo ya chakula nchini.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii