SERIKALI KUIMARISHA ELIMU YA KILIMO NA USALAMA WA CHAKULA NCHINI

Serikali imedhamiria kuimarisha elimu ya kilimo kwa kuwa ni nguzo muhimu katika kukabiliana na changamoto za usalama wa chakula na mabadiliko ya tabianchi na suala la ajira kwa vijana.

Amesema hayo Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Mweli Oktoba 15 mwaka huu wakati akigawa tuzo kwa wanafunzi na watumishi wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) waliofanya vyema kitaaluma katika utafiti na ubunifu mkoani Morogoro na kusema kuwa tuzo hizo ni ishara ya safari ndefu ya umahiri ubunifu na kujituma unaokipambanua Chuo cha SUA kama kitovu cha maarifa na mabadiliko.

Amesema kuwa chini ya Uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Serikali imeendelea kuwekeza katika programu mbalimbali za kuwajengea vijana uwezo katika kilimo ikiwemo programu za vijana na wanawake ya Jenga Kesho iliyo Bora (Build a Better Tomorrow program - BBT) SUA STEPS na Mpango wa Kukuza na Kuendeleza Kilimo Biashara (AIP).

Ameongeza kuwa programu hizo zimekuwa chachu kwa vijana kujiajiri kuwa wabunifu na kushiriki kikamilifu katika mnyororo wa thamani wa kilimo.

Katibu Mkuu Mweli ameongeza kuwa SUA ina jukumu kubwa si tu kwa Tanzania bali pia kwa Bara la Afrika katika kuzalisha wahitimu na watafiti wenye uwezo wa kuimarisha uzalishaji wa chakula na kuboresha mifumo ya chakula Duniani.

Hivyo ameihamasisha SUA kupitia upya mitaala yake ili kuendana na mahitaji ya soko la ajira la karne ya 21.

Naye Makamu Mkuu wa SUA Prof. Raphael Chibunda amesema kuwa zaidi ya wanafunzi na wanataaluma 180 wamefanya vizuri katika masomo tafiti na ubunifu mbalimbali na watatunukiwa zawadi kuanzia shilingi elfu 50 hadi milioni moja.

Amewapongeza wahitimu wote waliopata tuzo hizo na kueleza matumaini yake kwamba wataendelea kufanya vizuri na kuchangia katika kutatua changamoto za jamii wanazotoka.

Kwa upande wake Naibu Makamu Mkuu wa Chuo upande wa Taaluma ya Utafiti na Ushauri wa Kitaalam Prof. Maulid Mwatawala ameeleza kuwa utaratibu huo wa kutoa zawadi ni kuongeza ari na ufanisi katika masomo ya tafiti na ubunifu.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii