Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda ameitaka bodi mpya ya Bonde la ziwa Victoria kusimamia menejimenti ya bonde la ziwa hilo ili iwajibike ipasavyo katika kulinda rasilimali maji kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Mhe. Mtanda ametoa rai hiyo Oktoba 15 mwaka huu wakati akizindua bodi ya nane ya bonde hilo pamoja na vitendea kazi (Magari) kwa ajili ya matumizi ya bodi hiyo hafla iliyofanyika katika viwanja vya ofisi ya bonde hilo jijini Mwanza.
Mhe. Mtanda amesema katika kutekeleza majukumu yao wana wajibu wa kutoa elimu kwa jamii juu ya taratibu na sheria za matumizi ya rasilimali maji na sio kusubiri mwananchi akosee ndipo wamchukulie hatua hususani wanaochimba visima vya maji.
Aidha Mhe. Mtanda ameishukuru Serikali kwa kutoa Tshs.Bilioni 264.8 mkoani humo katika sekta ya maji ambazo zimetumika kuongeza upatikanaji wa maji mjini vijijini kutoka 58% hadi 85% na kutoka 53% hadi 77% kwa mjini huku akibainisha uwepo wa miradi kadhaa vijijini na mijini.
Akitoa salamu kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara, Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimali za Maji Bw. Robert Sande amesema bodi ya nane inaingia rasmi kufuatia kufikia ukomo wa bodi ya saba mwezi juni mwaka huu iliyodumu kwa miaka mitatu kutoka Disemba 03, 2022.
Ameongeza kuwa Dira ya Taifa ya 2050 inalenga kuifikisha nchi kwenye uchumi wa kati na imeelekeza kuwepo kwa rasilimaji maji ya kutosha na usimamizi wa rasilimali maji na eneo oevu hivyo bodi hiyo mpya ina jukumu la kutekeleza hayo pamoja kutekeleza sera mpya ya maji ya mwaka 2002 toleo la 2025.
Naye aliyekuwa Mwenyekiti wa bodi iliyomaliza muda wake Dkt. Boniventura Baya amesema bodi ya saba imepata hati safi mfululizo kutoka kwa CAG na kwamba wamefanya tathmini na ufuatiliaji wa uwingi na kuthibiti ubora na usalama wa rasilimaji za maji pamoja na kulinda vyanzo vya maji.