Utafiti unaoendelea kufanyika katika Kitalu cha Lindi–Mtwara, mkoani Mtwara umeonesha dalili za uwepo wa Gesi Asilia, hususani katika vijiji vya Mnyundo na Mpapura, mkoani Mtwara, ambapo visima vya maji vilibainika kuvujisha gesi asilia.
Utafiti huo unajumuisha jumla ya vijiji 48 katika eneo la takriban kilomita za mraba 736 ambapo vijiji 40 vinatoka katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara (Mtwara DC) na vijiji 8 ni kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mtama (Mtama DC).
Katika ziara yake ya kukagua miradi ya gesi na mafuta mkoani Mtwara, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio, amesema kuwa utafiti wa awali unaonesha uwezekano mkubwa wa kupatikana kwa gesi asilia katika eneo hilo.
“Kwa kutumia data za mitetemo zilizokusanywa awali, tumebaini kwamba kuna hadi asilimia 32 ya uwezekano wa gesi kuwepo katika kitalu hiki,” amesema Dkt. Mataragio.
Ameeleza kuwa mahitaji ya gesi yamekuwa yakiongezeka katika sekta mbalimbali zikiwemo viwanda, matumizi ya majumbani na usafirishaji – jambo linaloifanya Serikali kuendelea kuchochea utafutaji na uendelezaji wa vyanzo vya nishati hiyo ili kutimiza malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.
Katika ziara hiyo, Dkt. Mataragio pia alitembelea mradi wa kuongeza uzalishaji wa gesi katika eneo la Mnazi Bay, ambapo amebaini kuwa mradi huo uko katika hatua ya maandalizi kwa asilimia 68.
Mradi wa Mnazi Bay unahusisha visima vitatu vya gesi asilia, ambapo serikali inatarajia kuongeza uzalishaji kwa wastani wa futi za ujazo milioni 45 kwa siku kutoka kwenye visima viwili, huku kisima kimoja kikiwa ni kwa ajili ya utafiti zaidi wa uwepo wa gesi katika eneo lingine katika kitalu.