Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Ghana (Ghana Civil Aviation Authority -GCAA) ilitoa kibali kwa Air Tanzania kuanza safari za moja kwa moja baina ya Tanzania na Ghana katika hafla iliyofanyika katika Makao Makuu ya ofisi za GCAA, Jijini Accra.
Kibali hicho kilitolewa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa GCAA Mchungaji, Stephen Wilfred Arthur kwa Mhe. Selestine Gervas Kakele, Balozi Mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Ghana mwenye Makazi Abuja, Nigeria.
Vilevile, Mamlaka hiyo ilitoa Cheti cha Usafirishaji wa Bidhaa Hatari (Certificate for the Transportation of Dangerous Goods) ikithibisha Uthabiti wa viwango vya kimataifa vya utunzaji salama, upakiaji na usafirishaji wa bidhaa hatari kwenye Ndege unaofanywa na ATCL.
Kuanza kwa safari hizi za anga kutarahisisha huduma ya usafiri wa anga na kuchochea kukua kwa biashara, uwekezaji na utalii baina ya Tanzania na Ghana pamoja eneo zima la ukanda wa Afrika Magharibi.