Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita linamshikilia Martha Japhet (44), Mnyamwezi, mkulima na mkazi wa Kitongoji cha Mzalendo, Kijiji cha Mawemeru, Kata ya Nyarugusu, Wilaya ya Geita kwa tuhuma za mauaji ya mume wake aitwaye Shabani Paschal (55), kabila Muha, mkulima na mchimbaji madini.
Tukio la mauaji limebainika Oktoba 16 mwaka huu majira ya saa 7:00 mchana katika Kitongoji cha Mzalendo, baada ya taarifa kufikishwa Kituo cha Polisi majira ya saa 1:00 asubuhi siku hiyo hiyo, ikieleza kuwa Shabani Paschal hajaonekana nyumbani kwake tangu Oktoba 11 mwaka huu majira ya saa 3:00 usiku. Kufuatia taarifa hiyo, Jeshi la Polisi lilianza uchunguzi mara moja na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa Martha Japhet na kumhoji kwa mujibu wa sheria.
Katika mahojiano hayo, mtuhumiwa amekiri kuhusika katika tukio hilo na kueleza kuwa, alimshambulia mume wake kwa kutumia kitu chenye ncha kali sehemu ya kichwani. Baada ya kugundua kuwa amefariki, alichimba shimo ndani ya chumba walichokuwa wanalala, akamzika, akajaza kifusi cha udongo kisha kuweka magunia ya mihogo (udaga) juu yake ili kuficha ushahidi.
Uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha tukio ni migogoro ya kifamilia. Uchunguzi wa tukio hili unaendelea na mara baada ya kukamilika, mtuhumiwa atafikishwa mahakamani.
Jeshi la Polisi linawataka wananchi kuepuka kujichukulia sheria mikononi, na kuwataka kutoa taarifa mapema kuhusu viashiria vya migogoro au ukatili ili hatua stahiki zichukuliwe kwa wakati. Aidha, Jeshi la Polisi litaendelea kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wote watakaobainika kujihusisha na vitendo vya kihalifu.