MAABARA TANO ZA KITAIFA ZA KUPIMA UBORA NA UFANISI WA MATUMIZI YA NISHATI NA KIWANGO CHA CHINI CHA UFANISI WA MATUMIZI YA NISHATI ZAZINDULIWA
Serikali kwa kushirikiana na Jumuiya ya Umoja wa Ulaya( EU) imezindua maabara tano za Taifa zitakazopima Ubora na Ufanisi wa Matumizi bora ya Nishati pamoja na Kiwango cha Chini cha Ufanisi wa Matumizi ya Nishati pamoja na mfumo wa uwekaji alama za nishati.
Pia kimezinduliwa kifaa cha kupima kiwango cha hewa ya ukaa inayozalishwa katika majiko.
Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika Oktoba 16 mwaka huu jijini Dar es Salaam, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio amesema kuwa maabara hizo zimekuja kwa wakati sahihi kwa kuwa tayari Serikali inatekeleza sera na mikakati mbalimbali ya nishati nchini.
Maabara hizo pamoja na kifaa hicho cha kupima hewa ya ukaa vinapatikana katika Shirika la Viwango Tanzania (TBS).
Dkt. Mataragio amesema miradi hiyo italeta mabadiliko makubwa nchini katika matumizi bora ya nishati, Matumizi ya nishati safi ya kupikia, kuongeza juhudi za kutunza mazingira na kupunguza gharama za matumizi ya umeme kwa wananchi.
“Ni wakati wa kujivunia kama taifa tunapochukua hatua mahsusi kuhakikisha kila kifaa kinachotumika majumbani, maofisini, na viwandani kinachangia matumizi sahihi na yenye ufanisi wa nishati, na hii ni dhamira ya dhati ya serikali yetu kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji wa huduma za nishati za kisasa, nafuu, na salama kwa wote huku kukiwa na matumizi bora ya nishati kwa maendeleo ya kiuchumi na kijami." Amesema Dkt. Mataragio
Amesema kuwa maabara na Viwango vilivyozinduliwa vitahakikisha kuwa ni bidhaa zenye ubora na ufanisi pekee ndizo zinazoingia sokoni, hivyo kupunguza matumizi ya umeme, gharama kwa watumiaji, na uzalishaji wa hewa ya ukaa.
Utekelezaji wa mradi huo kwa pamoja vinachangia zaidi ya asilimia 45 ya matumizi ya umeme nchini kitaifa huku uwekaji wa viwango vya ufanisi unatarajia kuokoa zaidi ya 370 GWh za umeme kila mwaka kufikia 2030, sawa na kuupatia umeme zaidi ya nyumba 500,000 kila mwaka na kupunguza zaidi ya tani 250,000 za hewa ya ukaa (CO₂) kila mwaka.