Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha Bi. Amina Khamis Shaaban ameshiriki katika kikao cha Mawaziri wa Fedha kilichojadili namna ya kuongeza na kuharakisha upatikanaji wa fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa nchi zinazoendelea chini ya Uenyekiti wa Brazil wa COP30.
Bi. Amina amepongeza juhudi za Brazil kuanzisha COP30 Circle of Finance Ministers kama chombo muhimu cha kusukuma utekelezaji wa Mpangokazi wa Baku to Belem inayolenga kukusanya dola Trilioni 1.3 kwa mwaka ifikapo 2035 kwa ajili ya kukabiliana na masuala ya mabadiliko ya tabianchi.
Pia amesisitiza umuhimu wa kuimarisha uwezo wa ndani na kushirikisha sekta binafsi kupitia njia bunifu kama hati fungani za kijani (green bonds), blended finance, na carbon credits ili kuvutia uwekezaji zaidi katika miradi ya kijani.
Akihitimisha Bi. Amina ameihakikishia jumuiya ya kimataifa kuwa Tanzania iko tayari kushirikiana na nchi nyingine katika utekelezaji wa Mpangokazi wa Baku to Belem, akisisitiza kuwa uwekezaji katika tabianchi siyo gharama pekee, bali ni fursa ya ajira, ustahimilivu na ukuaji wa uchumi endelevu.
Mkutano wa Maandalizi ya COP30 kwa Mawaziri wa Fedha umefanyika wakati wa Mikutano ya Mwaka ya Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) inayofanyika Washington D.C Marekani.