Serikali ya Tanzania kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu imepokea ujumbe wa wataalamu kutoka Serikali ya Eswatini waliowasili nchini kwa lengo la kujifunza utekelezaji wa programu ya ukuzaji ujuzi, hususan mafunzo ya Uanagenzi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ajira na Ukuzaji Ujuzi Alana Nchimbi alisema kuwa ziara hiyo inalenga kuwapatia wataalamu hao maarifa ya kina kuhusu mbinu na mafanikio ya Tanzania katika kuwajengea vijana ujuzi wa vitendo.
“Ujumbe huu unatarajia kutumia maarifa Programu ya Ukuzaji Ujuzi kuboresha mpango wa Ujuzi wa Taifa lao,” amesema
Ujumbe huo umejumuisha wawakilishi kutoka Kituo cha Uchambuzi na Utafiti wa Sera ya Uchumi cha Eswatini pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu ambapo wataalamu hao walitembelea Taasisi ya Don Bosco ya Dodoma na kushuhudia kwa vitendo namna programu ya Uanagenzi inavyotekelezwa.
Aidha wakati wa ziara hiyo wageni hao walikagua karakana za mafunzo kwa kuzungumza na wanagenzi walioko katika mafunzo ya vitendo na kujionea kazi mbalimbali walizotengeneza.
Vile vile amesema kuwa mkakati wa Serikali wa kupunguza tatizo la ajira kwa vijana na kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia ujuzi wa vitendo Programu hiyo imekuwa chachu ya mabadiliko kwa maelfu ya vijana nchini.
Kwa upande wake Kiongozi wa ujumbe kutoka Eswatini Gcebile Dlamini amepongeza juhudi za Tanzania kwa kutekeleza programu hiyo ambayo imekuwa ni chachu ya kukuza ujuzi kwa nguvu kazi.
“Tumefurahishwa na namna Ofisi ya Waziri Mkuu inavyowekeza katika ujuzi wa vijana. Hii ni mfano bora wa kuigwa na nchi nyingine.”
Programu ya mafunzo ya Uanagenzi inayotekelezwa na Ofisi ya Waziri Mkuu inalenga kuwajengea vijana ujuzi katika fani mbalimbali zikiwemo ufundi umeme, useremala, uashi, teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA).
Hata hivyo Serikali hufadhili ada za mafunzo kwa kipindi cha miezi sita kwa kila mwanagenzi kwa kushirikiana na vyuo vya mafunzo nchini.