WANANCHI MKOANI GEITA WAHAKIKISHIWA ULINZI NA USALAMA KABLA, WAKATI NA BAADA YA UPIGAJI KURA

Vyombo vya ulinzi na usalama mkoani Geita vimeendelea kuimarisha ulinzi na usalama ili kuhakikisha amani, usalama na utulivu kabla, wakati na baada ya kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika Oktoba 29 mwaka huu.

Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama ya Mkoa wa Geita ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Martine Shigela, wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Senga, Wilaya ya Geita Oktoba 18 mwaka huu.

“Tunawahakikishia usalama wakati wa kupiga kura  Oktoba 29 mwaka huu Usalama upo na utakuwepo, na kila mwananchi aliyejiandikisha hatuzuiliwa kwenda kupiga kura.

Wananchi wa Mkoa wa Geita wajue kwamba vyombo vya dola vimejipanga kikamilifu kuhakikisha Watanzania waliojiandikisha wanakwenda kupiga kura bila bughudha wala hofu yoyote.

Nchi yetu ni ya amani, ni nchi ya usalama, na vyombo vya dola vimeimarishwa zaidi na vinawathamini Watanzania. Tunataka amani iendelee kutawala ili tuwapate viongozi.” Amesema Mhe. Shigela.

Kadhalika Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Geita SACP Safia Jongo amesisitiza kuwa Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama mkoani humo, limejiandaa na kujipanga kikamilifu kuimarisha ulinzi na usalama.

Ameongeza kuwa wananchi wasiwe na hofu yoyote, kwani hakutakuwa na mtu yeyote atakayewazuia wananchi kupiga kura na kuwataka kujitokeza kwa wingi kwenda kupiga kura.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii