Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko amewataka watendaji wa wizara ya Afya na wadau wa afya nchini kusimamia utekelezaji wa afua na misingi iliyoapangwa kwenye andiko la mradi wa Mfuko wa Dunia wa pamoja ili kufanikisha malengo yaliyopangwa.
Ametoa agizo hilo leo Oktoba 15 mwaka huu Mkoani Mwanza wakati wa Uzinduzi wa Mradi wa ‘Pandemic Fund’ unaolenga kuimarisha uwezo wa kuzuia, kujiandaa, kugundua, kukabiliana na kudhibiti magonjwa ya mlipuko na dharula nyingine za afya nchini kwa kushirikiana baina ya serikali na wadau wa maendeleo wa ndani na nje ya nchi.
Katika kufanikisha hayo Dkt. Biteko ameielekeza pia wizara ya Afya kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji wa magonjwa katika maeneo mbalimbali ya bianadamu na wanyama ili kubaini kwa haraka na kuchukua hatua na kusaidia kuimarisha afya kwa kulinda nguvu kazi ya bianadamu na wanyama na mifugo nchini.
Amesema kuwa magonjwa mbalimbali yamekuwa yakihatarisha maisha ya wataanzania na duniani kote hivyo ni jambo jema kwa taifa kuwa na mipango na mikakati ya kuhakikisha wanajiandaa kupambana na maradhi ya magonjwa ya milipuko kama Chikungunya, Ebola, Covid na Kipindupindu hivyo mfuko huo wa pamoja utaleta tija.
Akitoa salamu za Mkoa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe Said Mtanda amemshukuru Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa Tshs. Bilioni 63.2 ndani ya miaka minne zilizolenga kuboresha huduma ndani ya sekta ya afya.
Ameongeza kuwa katika kipindi hicho pia kumekua na ongezeko la fedha zilizotumika kununua dawa na vifaa kutoka Tshs. Bilioni 4 hadi 10.3 vituo vyenye uwezo wa kufanya upasuaji kutoka 17 hadi 45 pamoja na ongezeko la vifaa kama ‘Digital X-ray’ kutoka 2 hadi 26 na CT Scan ambazo hazikuwepo kabisa hadi kuwa nazo 4.