Mambo mapya yameibuka katika shauri la kutekwa kwa aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole, baada ya mawakili wake kuiomba Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam iridhie kupokea ushahidi wa mdomo wa Christina Polepole, ambaye ni dada wa Humphrey.
Maombi hayo yametolewa leo Oktoba 15 mwaka huu na Peter Kibatala, kiongozi wa jopo la mawakili wa Polepole wakati shauri lilipoitwa kwa ajili ya usikilizwaji.
Shauri hilo la maombi namba 24514/2025 linalosikilizwa na Jaji Mfawidhi, Salma Maghimbi lilifunguliwa na wakili Kibatala kwa niaba ya Polepole Oktoba 7 mwaka huu chini ya hati ya dharura, dhidi ya Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) na wenzake.
Wajibu maombi wengine kwa mfuatano ni Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) Mkuu wa Upelelezi wa Kanda Maalumu Dar es Salaam (ZCO) na Kamanda wa Polis Kanda Maalumu Dar es Salaam (ZPC).
Wakati shauri lilipotajwa Kibatala akishirikiana na mawakili Faraji Mangula na Gloria Ulomi, ameieleza mahakama kuwa leo asubuhi amepata taarifa kutoka kwa Christina, dada wa Polepole ambazo ni muhimu mahakama kuzifanyia kazi.