Mahakama Kuu Masjala Kuu Dodoma imeitupa kesi ya Luhaga Mpina na ACT-Wazalendo, ikieleza kwa mujibu wa Sheria na Katiba ya nchi, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) haipaswi kuingiliwa na chombo chochote kwa jambo ambalo ilifanya kwa nia njema.
Mpina alikuwa akipinga kuenguliwa katika nafasi ya kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29 mwaka huu.
Uamuzi huo umetolewa leo Jumatano Oktoba 15 mwaka huu mbele ya mahakama hiyo na kiongozi wa jopo la majaji wanaosikiliza kesi hiyo Jaji Fredrick Manyanda. Majaji wengine waliosikiliza kesi hiyo ni Sylvester Kainda na Abdallah Gonzi.
Kwa uamuzi huo Mpina hataweza kushiriki kinyang’anyiro cha uchaguzi mkuu, ambao kwa sasa vyama vya siasa vinavyoshiriki vinaendelea na kampeni.