Venezuela imetangaza kufunga balozi zake nchini Norway na Australia, na kufungua mpya katika mataifa ya Burkina Faso na Zimbabwe, ikisema ni sehemu ya “mabadiliko ya kimkakati” ya huduma za kidiplomasia.
Serikali ya Venezuela imetangaza kufunga ubalozi wake mjini Oslo, Norway, siku chache baada ya kiongozi wa upinzani Maria Corina Machado kutunukiwa Tuzo ya Amani ya Nobel. Katika taarifa iliyotolewa Jumatatu, serikali ya Caracas ilisema hatua hiyo ni sehemu ya "marekebisho ya huduma za kidiplomasia,” bila kutaja moja kwa moja tuzo hiyo. Venezuela pia imefunga ubalozi wake nchini Australia, huku ikifungua vituo vipya vya kidiplomasia Zimbabwe na Burkina Faso, mataifa ambayo imeyataja kuwa "washirika wa kimkakati katika kupinga shinikizo la kiukiritimba.”
Wizara ya mambo ya nje ya Norway ilithibitisha kufungwa kwa ubalozi huo, ikisema haikupewa sababu maalum. "Ni jambo la kusikitisha. Licha ya tofauti zetu, Norway inataka kuendelea na mazungumzo na Venezuela,” alisema msemaji wa wizara hiyo, Cecilie Roang, kupitia barua pepe kwa AFP. Kufikia Jumatatu jioni, huduma za simu za ubalozi wa Venezuela mjini Oslo zilikuwa zimekatwa.