Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imeonya watumiaji wa simu na mitandao kuacha tabia ya kukubali masharti (Terms and Conditions) kwenye programu tumizi (Applications) bila kusoma kwa kuwa inaweza kuhatarisha usalama wa taarifa binafsi.
Onyo hilo limetolewa wakati wa mafunzo ya usalama wa mtandao yaliyotolewa kwa walimu na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Pamba jijini Mwanza Oktoba 13 mwaka huu yaliyolenga kuongeza uelewa wa jamii kuhusu mbinu za wahalifu wa mtandao na namna bora ya kujilinda.
Akizungumza katika mafunzo hayo Bw. Yusuph Kileo mtaalam wa usalama wa mtandao alisema watumiaji wengi hukubali masharti ya programu mbalimbali wanazopakua na kutumia bila kufahamu madhara yake.
“Tabia ya kubofya viungo au kufungua programu zisizojulikana na kuruhusu vitu kwenye simu yako bila kusoma masharti ndipo hatari ya usalama wako wa mtandao unapoanzia,” alisema.
Awali Bw. Hafidhi Masoud Afisa TEHAMA kutoka Wizara hiyo alieleza mbinu zinazotumiwa na wahalifu wa mtandao ikiwemo kutuma barua pepe zenye viambatanisho hatarishi, kuiba taarifa binafsi, na kuunda tovuti bandia.
Naye Bi. Joseline Chambasi mtaalam kutoka Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi aliwakumbusha walimu kuwa makini na taarifa wanazoweka mitandaoni, hususan picha na mahali walipo, kwani vinaweza kutumiwa vibaya.