Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Ndg. Gerson Msigwa amefanya ziara ya kukagua Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam ambao umefikia asilimia 90 ya ukarabati.
Amefanya ziara hiyo Oktoba 13 mwaka huu akiwa ameongozana na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Ndg. Methusela Ntonda ambapo ukamilishaji huo ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita kuboresha miundombinu ya michezo nchini.
"Serikali inaendelea kusimamia kwa karibu ukarabati huo ili kuhakikisha viwango vya kimataifa vinazingatiwa na lengo ni kuona uwanja huu unarejea katika hadhi yake" alisema Msigwa.
Kati ya maeneo yaliyofanyiwa marekebisho ni pamoja na ufungaji wa taa mpya za kisasa, uwekaji wa nyasi bora za bandia (Pitch), marekebisho ya njia za kukimbilia (Running Track), ufungaji wa viti vipya, ukarabati wa vyoo, ufungaji wa milango mipya na uwekaji wa vigae vipya pembezoni mwa uwanja.