Wanawake Chunya wachangamkia fursa ya uchimbaji madini

Sekta ya Madini nchini Tanzania inaendelea kuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo ya kiuchumi na kijamii na sasa inajulikana kama Sekta jumuishi inayotoa nafasi sawa kwa wote, wanaume, wanawake na vijana kushiriki kikamilifu. Wanawake Wilayani Chunya ni ushahidi wa mabadiliko haya, wakivunja dhana ya zamani kuwa madini ni kazi ya wanaume pekee.

Wakizungumza na Madini Diary hivi karibuni, baadhi ya wanawake hao wameeleza jinsi wanavyoshiriki katika kila hatua ya mnyororo wa madini: wapo wanaomiliki leseni za uchimbaji mdogo, wachimbaji mahiri, wapondaji wa mawe na wafanyabiashara. Wanasema shughuli hizo zimewawezesha kupata kipato, kulea familia, kuanzisha miradi ya maendeleo na kujenga makazi bora.

Ushuhuda wao unaonesha wazi kuwa sekta ya madini inayoendeshwa kwa usawa wa kijinsia inaweza kuwa chachu ya mabadiliko chanya kwa jamii na taifa kwa ujumla.

Mwenyekiti wa Kikundi cha Wachimbaji Wanawake Itumbi-Chunya Happiness Mabula anasema “Mimi kwenda chini umbali wa mita 200 kuchimba madini ni kitu cha kawaida sana kwangu na nimefanya kazi hii si chini ya miaka 10, nina migodi yangu na nimekua nikilipa kodi kwa Serikali kwa miaka yote na tunawasaidia vijana. Anaongeza kwamba, kama wanawake wananufaika na shughuli za madini na hivyo kuisaidia jamii.

Licha ya mafanikio hayo anasema changamoto zipo kama kuvamiwa maeneo yao.

Naye Makamu Mwenyekiti wa kikundi hicho Angela Sompo anasema, ‘’kikundi chetu kilianza mwaka 2023 tukiwa wanawake 25, tulianza kwa kuwezeshana kwa kuchangiana vifaa kazi kama makarasha, compressor na mpaka sasa tumekwisha kutoa vifaa kwa wanachama 11 na vifaa hivi vimeturahisishia kazi zetu,’’ na anaongeza, ‘’tulianza kwa kuchangishana michango ya shilingi milioni 1 kila mwezi fedha zilizotusaidia kupata mitaji na kununua vifaa. Mbali na hayo, Angela anasema amekuwepo kwenye shughuli hizo kwa miaka 10 sasa, anachimba kwenye leseni za mume wake ambazo umempatia mafanikio ya kiuchumi.

Angela anasifu juhudi za Serikali kusimamia bei ya dhahabu na sasa wananufaika zaidi.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii